Al Ahly yatinga nusu fainali AFL, yaitoa Simba SC

© Kwa Hisani

KANDANDA Al Ahly yatinga nusu fainali AFL, yaitoa Simba SC

Zahoro Mlanzi • 19:42 - 24.10.2023

Simba sasa wanarudi nyumbani wakiwa wamejihakikishia kitita cha dola milioni 1 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 2.3 za Kitanzania.

Timu ya Al Ahly ya Misri, imetinga nusu fainali ya michuano ya AFL kwa bao la ugenini baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Simba SC katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Kimataifa wa Cairo nchini Misri.

Katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es Salaam, timu hizo zilifungana mabao 2-2, hivyo kufanya matokeo ya jumla kuwa mabao 3-3 lakini Al Ahly amesonga mbele kwa kunufaika na bao la ugenini.

Katika mchezo huo, Kocha wa Simba, Mbrazil Roberto Oliviera 'Robertinho', alianza kwa kuwapa heshima wapinzani wake na kuwaachia wabaki na mpira kwa muda mwingi lakini bila kuwa na madhara kwenye lango lao.

Mshangao wa mashabiki wengi wa soka nchini Tanzania, ilikuwa ni kuanzishwa kikosini kwa Nahodha mkongwe wa Simba, John Bocco ambaye alikuwa akiongoza safu ya ushambuliaji akisaidiwa na Kibu Denis na Saido Ntibanzokiza.

Wenyeji Al Ahly walijaribu kutengeneza nafasi nyingi lakini kikwazo ilikuwa ni safu ya ulinzi ya Simba iliyokuwa inaongozwa na Henock Inonga na Che Malone Fondoh waliokuwa imara kuondoa mauzauza yote yaliyoelekezwa langoni mwao.

Hadi Mwamuzi Jean Ndala anapuliza kipyenga cha kutamatisha dakika 45 za kwanza timu hizo zilikuwa suluhu.

Kipindi cha pili kilianza kwa Kocha Robertinho kufanya mabadiliko ya kumtoa Bocco na nafasi yake kuchukuliwa na Jean Baleke ambaye alileta uhai katika safu ya ushambuliaji wa timu hiyo.

Follow Pulse Sports Kenya WhatsApp channel for more news.

Simba ndio ilikuwa ya kwanza kufunga bao kupitia Sadio Kanoute dakika ya 68 baada ya mpira kumgonga kichwani na kujaa wavuni akiwa katika harakati za kukwepa mpira wa kichwa uliopigwa na Ntibazonkiza, hata hivyo, Mahmoud Kahraba wa Ahly, alisawazishia timu yake dakika chache baadaye.

Kiungo mshambuliaji wa Al Ahly, Percy Tau, amejikuta akipoteza nafasi nyingi nzuri za kufunga kama ilivyokuwa kwenye mechi ya kwanza kwa kukosa umakini anapolikaribia goli.

Simba sasa wanarudi nyumbani wakiwa wamejihakikishia kitita cha dola milioni 1 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 2.3 za Kitanzania.