Azizi KI apiga 'Hat trick', Yanga ikiifunga Azam 3-2

© Kwa Hisani

KANDANDA Azizi KI apiga 'Hat trick', Yanga ikiifunga Azam 3-2

Zahoro Mlanzi • 21:16 - 23.10.2023

Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, umeifanya Yanga kupanda kileleni mwa msimamo wa ligi.

Kiungo mshambuliaji wa timu ya Yanga SC, Stephane Azizi KI, ameifungia mabao matatu 'Hat trick' timu yake ya Yanga SC katika ushindi wa mabao 3-2 walioupata dhidi ya Azam FC katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara.

Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, umeifanya Yanga kupanda kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo wakiwa na alama 15 sawa na Simba SC ila zinatofautiana kwa mabao na Azam kushuka hadi nafasi ya tatu na alama zao 13.

Shujaa wa Yanga katika mchezo huo ni Aziz Ki ambaye amefunga mabao yote matatu na kuwafanya wananchi kuendelea kuwatambia Azam kwa msimu wa tatu mfululizo.

Yanga ndio wamekuwa wa kwanza kuandika bao likifungwa dakika ya 8 na Aziz Ki ambaye alipokea pasi ndefu kutoka kwa Bakari Mwamnyeto na kisha kumlamba chenga mlinzi mmoja na kufunga bao safi kwa kumpiga tobo Kipa, Idrissu Abdullah.

Kuingia kwa bao hilo, kumewaamsha Azam ambao walianza taratibu na ilipofika dakika ya 18 walisawazisha bao hilo kupitia kwa winga wao, raia wa Gambia, Gibril Silla ambaye alifanya kazi ya ziada kuwalamba chenga walinzi wa Yanga na kupiga shuti kali nje ya boksi ambalo lilimshinda mlinda lango, Djigui Diarra.

Kuingia kwa mabao hayo kumezifanya timu zote zianze kusaka bao la pili lakini jitihada za makipa wa timu zote mbili zilifanya mchezo huo kwenda mapumziko matokeo yakiwa 1-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa Azam, kushambulia mfululizo na kupata bao la pili dakika ya 60 lililofungwa na Prince Dude kwa mkwaju wa penalti baada ya Mwanyeto kumuangusha Sillah ndani ya eneo la hatari.

Hata hivyo, bao hilo halikudumu zaidi ya dakika tano kwani Aziz Ki tena aliwarejesha Yanga mchezoni kwa kuchomoa bao hilo kwa shuti kali la mpira uliokufa ambalo liliwaamsha wananchi uwanjani hapo.

Aziz Ki alikamilisha hat trick yake kwenye mchezo huo baada ya walinzi wa Azam kuzubaa kuokoa mpira ambao ulikuwa unazagaa mbele ya goli lao na kumuacha raia huyo wa Ivory Coast kufunga bao safi nje ya boksi kufanya matokeo kuwa 3-2.

Feisal Salum ambaye msimu uliopita alikuwa Yanga kabla ya kujiunga Azam, alionesha uwezo mkubwa kwenye mchezo huo na kama si uimara wa viungo Khalid Aucho na Mudathir Yahaya basi wananchi wangekuwa matatizoni.

Huo unakuwa ni mchezo wa kwanza kwa Azam kupoteza kwenye ligi msimu huu ambapo hadi sasa wameshuka dimbani mara sita.