Manula abaki Dar Simba ikitua Misri

FOOTBALL: Manula abaki Dar Simba ikitua Misri

Na Zahoro Mlanzi • 16:30 - 22.10.2023

Manula na Kramo wote kwa pamoja hawajashiriki mechi yoyote ya kimashindano msimu huu.

Kikosi cha timu ya Simba SC, kimewasili salama nchini Misri kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mechi ya marudiano ya michuano ya AFL dhidi ya Al Ahly katika mchezo unaotarajiwa kupigwa kesho Uwanja wa Kimataifa wa Cairo.

Simba imesafiri na wachezaji 24 lakini matumaini ya mashabiki wa Simba kumuona mlinda lango wao namba moja, Aishi Manula yamezama baada ya kipa huyo kutokuwa sehemu ya wachezaji waliosafiri.

Hiyo inakuwa si habari njema kwa mashabiki wa Simba ambao wanahitaji timu yao iweze kusonga mbele baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Ijumaa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Dhamana ya Simba sasa ipo kwa walinda mlango, Hussein Abel, Ayoub Lakred na Ally Salim ambaye alidaka kwenye mchezo wa kwanza.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika mtandao wa klabu hiyo, mbali na Manula, mchezaji mwingine ambaye hajasafiri ni Aubin Kramo ambaye anasumbuliwa na majeraha tangu alipojiunga na Simba akitokea Asec ya Ivory Coast.

Manula na Kramo wote kwa pamoja hawajashiriki mechi yoyote ya kimashindano msimu huu lakini kwa mujibu ripoti za kitabibu ni kwamba wachezaji hao wanakaribia kurudi uwanjani.

Wachezaji walioondoka ni mabeki, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Israel Mwenda, Hussein Kazi, Kennedy Juma, Che Malone Fondoh, David Kameta na Henock Inonga.

Viungo ni Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute, Mzamiru Yassin, Saido Ntibazonkiza, Willy Onana, Clatous Chama, Abdallah Hamis na Luis Miquissone.

Washambuliaji ni Jean Baleke, Mosses Phiri, Denis Kibu, John Bocco na Shabaan Chilunda.

Tags: