Advertisement

Elvis Rupia aibeba Singida dhidi ya Future FC kutoka Misri

Mshambulizi huyo hatari alisajiliwa majuzi kutoka Kenya.
Advertisement

Bao pekee lililofungwa na Mkenya, Elvis Rupia, limeiwezesha timu ya Singida Fountain Gate, kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Future FC katika mchezo wa Kombe la Shirikisho.

Advertisement

Rupia ambaye msimu uliopita ameng'aa akiwa na Polisi ya Kenya, alifunga bao hilo kwa shuti kali akiwa ndani ya eneo la hatari baada ya kukutana na mpira uliokolewa vibaya na mabeki wa Future, waliokuwa katika harakati za kuucheza mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Marouf Tchakei.

Ushindi huo umeifanya Singida FG kuwa na mtaji mzuri kuelekea mchezo wao wa marudiano utakaopigwa mwishoni mwa mwezi huu nchini Misri.

Timu hizo hadi zimeenda mapumziko zilishindwa kufungana uwanjani Azam Complex, Dar es Salaam, licha ya Singida kunufaika na mashabiki wengi waliojitokeza uwanjani hapo.

Advertisement

Katika dakika hizo, timu zote zilipiga mashuti mawili mawili yaliyolenga kwa nyakati tofauti.

Kipindi cha pili, Singida imeongeza nguvu na ilitumia dakika tatu kubisha hodi langoni mwa Future kupitia kwa Kasengi Kazadi ambaye alipiga kichwa kilichopanguliwa na Kipa Mahmoud Abd akiunganisha krosi ya Gadiel Michael.

Dakika ya 51, Rupia ambaye msimu uliopita alikuwa Mfungaji Bora katika Ligi Kuu ya Kenya, amefunga bao hilo pekee ikiwa ni salamu kwa timu zingine hususani za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Advertisement

Rupia alisajiliwa na Singida FG hivi karibuni akitokea Polisi ya Kenya ambayo aliifanyia makubwa kwa kufunga zaidi ya mabao 25.

Katika mchezo huo, Rupia alionesha kiwango kizuri huku akishirikiana vizuri na Duke Abuya ambaye msimu uliopita wote walikuwa wakiichezea Polisi na wote waliitwa timu ya Taifa ya Kenya (Harambee Stars) iliyocheza mechi za kufuzu AFCON 2023 hivi karibuni.

Advertisement