Kocha wa timu ya Simba SC, Abdelhak Benchikha, amesema amefurahishwa na kiwango kilichooneshwa na wachezaji wake lakini hajaridhika na matokeo ya suluhu waliyopata dhidi ya Jwaneng Galaxy kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mchezo huo wa Kundi B ulipigwa nchini Botswana, ulikuwa ni wa pili kwa kila timu na ulikuwa ni wa kwanza kwa kocha huyo kuiongoza Simba kama kocha mkuu baada ya kujiunga nao mapema wiki iliyopita.
Akizungumza baada ya kutua salama Dar es Salaam, wakitokea Botswana, Benchikha amesema timu yake ilikuwa na nafasi ya kushinda mchezo huo kutokana na nafasi walizotengeneza lakini bahati haikuwa yao na hawakuweza kutumia nafasi walizopata.
Kocha huyo amesema licha ya kuwa hawakupata ushindi lakini ameona hali ya kujituma kwa wachezaji wake na anaamini kama wataendelea na hali hiyo katika michezo inayofuata basi wana nafasi ya kufanya vizuri zaidi.
"Tumetengeneza nafasi lakini tumeshindwa kuzitumia na hicho ndo kimefanya tushindwe kupata ushindi, hii ni hali ya kawaida kwenye mchezo," alisema.
"Kiwango ambacho kimeoneshwa na wachezaji wangu kimenipa matumaini, wachezaji wamejituma na kujitolea kwa ajili ya timu, hiyo imenipa imani kuwa tunaweza kufanya vizuri zaidi kama tutaendelea kushirikiana kama hivi," alimalizia Benchikha.
Kwa matokeo waliyopata Simba, sasa wapo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Kundi B wakiwa na alama 2 huku Asec Mimosa na Jwaneng Galaxy wote wakiwa na alama 4. Wydad wanaburuza mkia wakiwa hawana alama yoyote baada ya mechi mbili.
Simba mechi yao inayofuata katika kundi hilo itakuwa ni Desemba 9 ambapo watakuwa ugenini kucheza na Wydad nchini Morocco na kisha Desemba 19 watawakaribisha Wydad kwa Mkapa katika mchezo wa nne.
Wakati huo huo, Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), limeiondolea adhabu Klabu ya Simba ya kufungiwa kusajili wachezaji baada ya kuilipa Klabu ya Teungueth ya nchini Senegeal.
Awali FIFA wamewafungia Simba kwa kushindwa kuilipa klabu hiyo sehemu ya malipo ya mauzo ya mchezaji Pape Sakho. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) nao wamewafungulia Simba.