Sopu, Metacha waachwa kikosi cha mwisho Taifa Stars
Kocha Mkuu wa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Adel Amrouche, ametangaza jeshi la wachezaji 27 ambao wataiwakilisha nchi hiyo katika michuano ya Afcon Ivory Coast huku wachezaji, Metacha Mnata wa Yanga na Abdul Seleman 'Sopu' wa Azam wakiachwa.
Kikosi cha Stars ambacho kiliondoka nchini mwanzoni mwa wiki iliyopita kwenda kuweka kambi Misri, kiliondoka na wachezaji 31 lakini kwa mujibu wa kanuni za mashindano wachezaji wanaohitajika ni 27.
Mara baada ya kufanya maandalizi ya takribani siku tano Kocha, Amrouche alikuja na uamuzi wa kuwapunguza wachezaji wanne ambao ni Kipa, Metacha, Sopu, Twariq Seif na Khelfin Hamdoon 'Fini'.
Akizungumzia maandalizi ya kikosi hicho, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Hemed Morocco, amesema wachezaji wote tayari wapo kambini na wanaendelea na maandalizi vizuri kama walivyopanga ratiba zao.
Amesema wachezaji wameonesha kuwa na mwitiko mkubwa na wanahitaji kufanya vizuri kwenye michuano hiyo ambayo inaanza Januari 13.
"Maandalizi yetu yanaendelea vizuri, wachezaji wote tuliowaita wapo kambini na hakuna mwenye tatizo, kikosi kinaonesha nia ya kupambana kwakweli tunajivunia," amesema.
Stars itacheza mchezo wa kwanza Januari 17 dhidi ya Morocco kisha Januari 21 itacheza na Zambia na Januari 24 watamalizia kwa kucheza na DR Congo.
Kikosi kamili: Aishi Manula, Kwesi Kawawa, Beno Kakolanya, Ibrahim Abdullah Bacca, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Mohamed Hussen, Haji Mnoga, Abdi Banda, Lusajo Mwaikenda, Novatus Dismas, Abdulmalik Zakaria, Miano Danilo.
Wengine ni Himid Mao, Feisal Salum, Tarryn Allarakhia, Mourice Abraham, Mzamiru Yassin, Sospter Bajana, Mudathir Yahaya, Kibu Denis, Mohamed Omar, Cyprian Kachwele, Ben Starkie, Charles M'mombwa, Simon Msuva na Mbwana Samatta.