Hivi ndivyo Taifa Stars ilivyocheza na DR Congo

Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta (kushoto), akimpiga chenga Arthur Masauku wa DR Congo

KANDANDA Hivi ndivyo Taifa Stars ilivyocheza na DR Congo

Zahoro Juma • 11:52 - 25.01.2024

Ni tathmini ya jinsi nyota wa Taifa Stars walivyovuja jasho katika mchezo huo

Timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', kwa mara ya tatu katika historia yao ya kushiriki michuano ya AFCON imeshindwa kutinga hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo

Kwa mara ya kwanza Stars kufuzu kwa fainali hizo ilikuwa mwaka 1957 na ikaja kufuzu tena 2019 kabla ya kucheza tena kwa michuano ya 2023 ambayo imefanyika mwaka huu nchini Ivory Coast.

Katika michuano hiyo, Stars haijawahi kushinda mchezo wowote zaidi ya kuambulia sare kama ilivyofanya katika michuano ya mwaka huu.

Stars ilianza michuano ya mwaka huu kwa kufungwa mabao 3-0 na Morocco kabla ya kuja kutoka sare ya bao 1-1 na Zambia na kutoka suluhu na DR Congo.

Matokeo hayo, yameifanya Stars kumaliza Kundi F ikiwa mkiani kwa alama 2 sawa na Zambia ila DR Congo ikamaliza ikiwa na alama 3 na Morocco ikamaliza kinara kwa alama 7.

Hivi ndivyo wachezaji wa Taifa Stars walivyocheza dhidi ya DR Congo katika mechi hiyo ya mwisho na alama zao walizovua;

Aishi Manula-7

Ndiye kipa chaguo la kwanza ndani ya kikosi hicho na kwa Klabu yake ya Simba SC kwa zaidi ya miaka mitano sasa na amekuwa na mwendelezo mzuri kikosini.

Mashabiki walioangalia mchezo huo, hawana budi kusifia shuti alilopangua kutoka kwa Yoane Wissa dakika ya 77 na kuwa kona isiyokuwa na madhara.

Lakini pia alifanya kazi kubwa ya kuwapanga mabeki wake kuwa imara kuondosha hatari na kama si jitihada zake binafsi kutokea na kudaka mpira uliokuwa umeguswa kidogo na Fiston Mayele basi hadithi ingekuwa nyingine.

Lusajo Mwaikenda-6

Ni beki wa kulia ambaye anakipiga ndani ya Azam FC, tangu apewe nafasi kucheza badala ya Hajji Mnoga katika mchezo wa kwanza dhidi ya Morocco, ameaminika na kuanza katika mechi mbili zilizofuata.

Mwaikenda ana sifa ya kukaba vizuri na kupandisha mashambulizi lakini pia ana uwezo mzuri wa kupiga krosi zenye madhara.

Katika mchezo huo, alitoa ushindani mkubwa kwa winga Wissa ambaye alikuwa tishio katika safu ya ulinzi ya Stars.

Mohamed Hussein-7

Wakati akiachwa katika baadhi ya michezo ya kufuzu kwa Kombe la Dunia na AFCON, ilizua mjadala katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

Wapo walioamini uwezo wake umeshuka lakini wengine waliamini bado ana uwezo na hilo amekwenda kulithibitisha katika michuano hiyo kwa kuanza upande wa beki wa kushoto katika mechi zote tatu za hatua ya makundi.

Lakini pia amekuwa msaada mkubwa katika timu yake ya Simba kwa zaidi ya miaka 6 kwa sasa na hajawahi kuwekwa benchi akiwa si majeruhi.

Katika mchezo huo, amefanya kila linalotakiwa kufanywa kwa kuzuia na kuongeza nguvu katika kushambulia na kama angekuwa makini katika upigaji wa pasi za mwisho angeisaidia zaidi timu yake kupata mabao.

Ibrahim Abdullah-8

Tangu asajiliwe na Yanga msimu uliopita, nyota huyo kutoka visiwani Zanzibar amekuwa na mwendelezo mzuri na kujikuta akijitengenezea ufalme ndani ya Yanga na Taifa Stars.

Uwezo wake wa kukaba, kuondosha hatari za mipira ya juu, kupiga pasi ndefu ndicho kitu kinachomtofautisha na mabeki wengine wa kati nchini Tanzania.

Hakuna kocha ambaye anatamani kumuweka benchi beki huyo wa kati mwenye mapafu ya mbwa.

Kuna wakati Mayele alikuwa akikerwa na kumsukuma beki huyo kutokana na kutompa nafasi hata ya kupumua.

Amekuwa akishirikiana vizuri na Bakari Mwamnyeto kitu kinachowafanya kuendeleza upacha wao popote watakapoitwa kucheza pamoja.

Alimkataba straika huyo wa zamani wa Yanga ambaye kwa sasa anakipiga Pyramids ya Misri hadi alitolewa dakika ya 77 na nafasi yake kuchukuliwa na Cedric Bakambu.

Anatajwa kuwa Beki Bora wa kati kwa sasa katika soka la Tanzania.

Bakari Mwamnyeto-7

Ni beki asiyekuwa na makuu uwanjani. Si muongeaji lakini anafanya kazi yake kwa umakini mkubwa.

Tangu asajiliwe na Yanga akitokea Coastal Union misimu miwili iliyopita, amejikuta akijijengea heshima kubwa ndani ya kikosi cha Yanga hadi kupewa unahodha.

Ni beki mzuri katika mipira ya juu, ana nguvu na uwezo wa kupiga mipira ya mbali lakini si beki mwenye kasi.

Ameshirikiana vizuri na Abdullah katika kuhakikisha wanalilinda vizuri lango lao na Manula hapati shida katika kuondosha hatari.

Himid Mao-5

Ndiye mchezaji ambaye iliaminika ataifanya kazi yake vizuri ya kukata umeme eneo la katikati akiwa na jukumu kubwa na kuwalinda mabeki wake akicheza kama namba 6.

Ni mchezaji mwenye uzoefu wa kucheza mechi za kimataifa kwani amehudumu ndani ya kikosi cha Stars kwa zaidi ya miaka 7 na kwa sasa anacheza soka lake la kulipwa ndani ya Ghazi El Mahalla ya Misri.

Katika mchezo huo, ilionekana kutoamka vizuri kwani muda mwingi alikuwa akipewa changamoto kubwa na Gael Kakuta kwa kupitwa au kukaa na mpira hadi anapolwa.

Ameaminiwa na benchi la ufundi la Stars kwani alianza katika mechi zote tatu za hatua ya makundi licha ya kwamba hamalizi dakika zote 90.

Hajji Mnoga-6

Mchezaji huyo kiraka amekuwa na mwendelezo mzuri katika michuano hiyo kwa kucheza mechi mbili kati ya tatu katika michuano hiyo.

Ni mchezaji mwenye uwezo wa kucheza beki wa kulia au kiungo wa kati na katika mchezo huo alianza kama winga wa kulia lakini anayecheza katikati zaidi.

Alisaidia kwa kiasi kubwa katika kusaidia eneo la kiungo pamoja na beki wake wa kulia na kumfanya Wissa kuwa na wakati mgumu katika kulishambulia lango la Stars.

Novatus Dismas-7

Ni mchezaji mwingine kiraka mwenye uwezo wa kucheza beki wa kushoto na kiungo mkabaji na katika michuano hiyo alikosa mchezo mmoja dhidi ya Zambia kutokana na kutumikia adhabu ya kadi nyekundu.

Nyota huyo anayekipiga Shakhtar Donetsk ya Ukraine, amekuwa na msaada mkubwa ndani ya Stars kutokana na uwezo wake kukaa na mpira na kupiga pasi za uhakika.

Ni mzuri katika kupandisha mashambulizi na katika mchezo huo alikuwa alitoa sapoti kubwa kwa upande wa kushoto na kumpa wakati mgumu beki, Gedeon Kalulu ambaye baadaye alifanyiwa mabadiliko.

Mbwana Samatta-7

Ni nahodha wa Taifa Stars kwa muda mrefu na ndiye mchezaji mwenye mafanikio makubwa nchini Tanzania katika soka la sasa.

Kama ukizungumzia soka la Tanzania kwa sasa unamzungumzia Samatta kwani kucheza kwake soka la kulipwa katika Klabu za KRC Genk na Royal Antwerp za Ubelgiji, Aston Villa ya England na sasa anakipiga PAOK FC ya Ugiriki, yamekuwa mafanikio makubwa nchini.

Ndiye mchezaji anayeshika nafasi ya pili katika upachikaji mabao wa muda wote ndani ya Taifa Stars akiwa na mabao 22 sawa na Simon Msuva huku Mrisho Ngassa akiwa kinara kwa mabao 25.

Uwepo wake ndani ya Stars umekuwa ukiwapa presha mabeki wengi wa timu pinzani kwani muda mwingi wanakuwa wakimtolea macho.

Katika mchezo huo, alikuwa akibadilishana nafasi ya ushambuliaji na nyota wenzake katika kulishambulia lango la DR Congo.

Pamoja na hayo amekuwa akikosolewa kucheza bila kujituma kitu ambacho mashabiki wanaamini anaweza kuleta madhara zaidi ya anavyocheza kwa sasa.

Feisal Salum-6

Kama unamzungumzia namba 10 bora kwa sasa katika soka la Tanzania huwezi kulitaja jina na kiungo huyo mshambuliaji wa Azam FC.

Ana uwezo wa kupiga mashuti ya mbali yenye kulenga goli na ndio mabao yake mengi akifunga kwa staili hiyo.

Amekuwa akiunganisha vizuri safu ya kiungo na ya ushambuliaji wa Stars lakini amekosa nguvu za kimapambano anapokutana na wachezaji wenye misuli mikubwa.

Ana akili na ufundi wa kucheza mpira na ndicho kitu kinachomfanya apate nafasi ya kucheza katika kikosi hicho na timu yake ya Azam.

Simon Msuva-8

Ndiye straika tegemeo kwa sasa ukiacha Samatta na katika michuano hiyo ndiye mchezaji pekee ambaye amefunga bao kwa upande wa Stars.

Ubora wa kiwango chake, kujituma na kujitoa kumemfanya awe anazungumzwa sana na mashabiki wa soka nchini huku akilinganishwa na Samatta.

Nyota huyo silaha yake kubwa ni kasi, ana nguvu na uwezo wa kupiga mashuti na hujitoa sana anapokuwa uwanjani bila kujali chochote.

Bao lake hilo limemfanya kumfikia Samatta katika upachikaji mabao wa muda wote ndani ya kikosi cha Stars.

Akitokea kuvunjiwa mkataba wa JS Kabylie ya Algeria mwezi uliopita, nyota huyo juzi ametambulishwa kusajiliwa na Al-Najma ya Daraja la Kwanza nchini Saudi Arabia.

Hao ndio nyota waliaonza katika kikosi cha kwanza ila waliingia Mzamiru Yassin, Charles M'mombwa, Kibu Denis na Morice Abraham ambapo hata hivyo hakuna ambaye alionesha maajabu makubwa kutokana na muda mchache waliopewa.