Taifa Stars yaishia makundi AFCON

Mchezaji kiraka wa Taifa Stars, Hajji Mnoga (kushoto), akiwania mpira na Arthur Masauku wa DR Congo

KANDANDA Taifa Stars yaishia makundi AFCON

Zahoro Juma • 05:30 - 25.01.2024

Ni baada ya kutoka suluhu na DR Congo na kujikuta ikishika mkia katika Kundi F ikiwa na alama 2 sawa na Zambia

Timu ya soka ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', imetupwa nje ya michuano ya Afcon baada ya kulazimishwa suluhu na DR Congo kwenye mchezo wa mwisho wa Kundi F.

Matokeo hayo, yanawafanya Stars kumaliza michuano hii wakiwa na alama mbili na kuburuza mkia wa katika kundi hilo.

Stars ilianza michuano ya Afcon kwa kupokea kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Morocco kabla ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Zambia.

Alama 2 kwa Stars ni rekodi yao mpya katika michuano hiyo kwani katika mara zote mbili ambazo wamewahi kushiriki hakuna mwaka ambao wamevuka alama moja.

Katika mchezo dhidi ya DR Congo, Stars ilitakiwa kupata ushindi ili kujikatia tiketi ya 16 Bora.

Hata hivyo, Stars ilionekana kucheza kwa nidhamu kubwa ya kukaba uwanjani bila kuwa na madhara makubwa kwenye lango la DRC ambao wao hata sare kwao ilikuwa inatosha.

Kwa kupata suluhu hiyo, DR Congo wao wamefuzu wakishika nafasi ya pili baada ya kukusanya alama 3 kwa kutoka sare katika michezo yao yote ya makundi.

Timu ya Zambia ambao nao walifungwa na Morocco katika mchezo mwingine wa kundi hilo nao wamefungashiwa virago wakibaki na alama 2.

Katika mchezo huo, timu zote hazikutengeneza nafasi za wazi moja kwa moja kwani kipindi kirefu mchezo ulichezwa eneo la katikati ya uwanja.

Timu zilizoingia kwa kupitia 'best looser' ni Namibia na Guinea kwa kujikusanyia alama 4 kila moja zikifuatiwa na Mauritania na wenyeji Ivory Coast wenye alama 3 kila mmoja.