Taifa Stars karata muhimu leo ikiivaa DR Congo

Wachezaji wa Taifa Stars, Kibu Denisi (kulia) na Abdi Banda, wakiwa mazoezini

KANDANDA Taifa Stars karata muhimu leo ikiivaa DR Congo

Na Zahoro Juma • 14:02 - 24.01.2024

Huo ni mchezo wa mwisho wa Kundi F ambao ndio utatoa hatma ya timu hiyo kuendelea kuwepo katika mashindano ya AFCON

Hatma ya timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' katika michuano ya AFCON 2023, itajulikana leo saa 5 usiku wakati itakaposhuka uwanjani kuumana na DR Congo katika mchezo wa mwisho wa Kundi F.

Pia muda huo, Morocco ambayo inaongoza kundi hilo ikiwa na alama 4,itakuwa uwanjani kuumana na Zambia yenye alama 2 sawa na DR Congo katika mchezo mwingine wa kundi hilo.

Taifa Stars itacheza mchezo wake huo wa mwisho uwanjani Amadou Gon Coulibaly uliopo Mji wa Korhogo nchini humo.

Ikiwa inashika mkia katika kundi hilo, Stars imevuna alama 1 katika mechi mbili ilizocheza baada ya kufungwa na Morocco mabao 3-0 na kisha kutoka sare ya bao 1-1 na Zambia.

Timu zote katika kundi hilo zina nafasi ya kusonga mbele na hata pia zipo katika nafasi nzuri ya kuwania 'best looser' kama ilivyo katika makundi mengine.

Ushindi kwa Stars katika mchezo huo, utawahakikishia alama 4 ambazo bila shaka zitakuwa zimewavusha kuingia aidha moja kwa moja kulingana na matokeo ya mechi nyingine katika kundi hilo au kuingia kwa 'best looser'.

Stars bado inasaka ushindi wao wa kwanza katika michuano hiyo baada ya kufanikiwa kushiriki mara tatu 1980, 2019 na mwaka huu lakini wameambulia sare mara mbili tu na vipigo sita zote ikiwa ni katika hatua ya makundi.

Katika mchezo uliopita Stars ilikuwa chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Hemed Seleman 'Morocco' ambaye alichukuwa nafasi mara baada ya Kocha Mkuu, Adel Amrouche kufungiwa mechi nane na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Taifa Stars inaweza kumkaribisha tena kikosini mchezaji wao kiraka anayekipiga Shakhtar Donetsk, Novatus Dismas ambaye alikosa mchezo dhidi ya Zambia baada ya kuoneshwa kadi nyekundi katika mchezo wa kwanza dhidi ya Morocco.

Katika mechi 6 za mwisho kati ya Tanzania na DR Congo, kila timu imemfunga mwenzie mara mbili huku pia sare zikiwa mbili.

Mara ya mwisho walikutana katika michuano ya kufuzu Kombe la Dunia Novemba 11, 2021 ambapo Stars ilikubali kichapo cha mabao 3-0 nyumbani.

Katika mchezo huu wa leo, Kocha Seleman anatarajia kuanza na Kipa, Aishi Manula, mabeki ni Lusajo, Mwaikenda, Mohamed Hussein, Ibrahim Abdullah 'Bacca' na Bakari Mwamnyeto, Viungo ni Novatus, Himid Mao, Feisal Salum na Kibu Denis na washambuliaji ni Mbwana Samatta na Simon Msuva.

Tags: