AFCON 2023: Kocha Taifa Stars aahidi ushindi kwa Zambia

Makocha wa timu ya timu ya Tanzania ' Taifa Stars', Hemed Morocco (kushoto) na Juma Mgunda

KANDANDA AFCON 2023: Kocha Taifa Stars aahidi ushindi kwa Zambia

Na Zahoro Juma • 20:33 - 20.01.2024

Huo ni mchezo wa pili kwa timu hizo kutoka Kundi F linaloongozwa na Morocco yenye alama 3

Kaimu Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ' Taifa Stars' Hemed Seleman 'Morocco', amesema wamefanyia kazi kasoro zilizojitokeza katika mchezo wao wa kwanza wa AFCON na ameahidi kufanya vizuri dhidi ya Zambia kesho.

Stars katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya Morocco, ilipoteza kwa mabao 3-0 na kujikuta ikishika mkia katika Kundi F.

Morocco inaongoza kundi hilo ikiwa na alama 3 ikifuatiwa na DR Congo na Zambia zenye alama 1 kila moja na Stars ikiwa haina alama.

Akizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari, kocha Seleman amesema katika mazoezi ya mwisho ndio yatakayotoa taswira ya mchezaji gani ataanza na yupi atakaa benchi.

"Kiukweli kufungwa kunauma, tumeshafanyia kazi upungufu uliojitokeza katika mchezo wetu wa kwanza na sasa nguvu na akili zetu katika mchezo ujao, ule umeshapita," amesema Seleman.

Amesema kwa sasa vijana wapo tayari kupambana na Zambia kiakili na kimwili ila kikubwa anawaomba Watanzania kuendelea kuwaombea dua nzuri wapate matokeo.

Mchezo wa raundi ya pili unatarajiwa kucheza kesho saa 2 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na Kati uwanjani Stade Laurent Pokou, Ivory Coast.

Kabla ya mchezo huo, Morocco itashuka uwanjani saa 11 jioni kuumana na DR Congo.

Katika hatua nyingine, Kocha Juma Mgunda, ameungana na Morocco katika kuinoa timu hiyo baada ya Adel Amrouche kufungiwa mechi nane na CAF huku TFF pia ikimsimamisha kwa muda usiojulikana.

Mgunda ambaye ni Kocha Mkuu wa timu ya Simba Queens, si mara ya kwanza kuinoa Taifa Stars, kwani alishawahi kuwa Msaidizi wa Kocha, Ettiene Ndayiragije mwaka 2021.