Kocha Benchikha ataka straika mpya Simba

Kocha wa Simba SC, Abdelhak Benchikha, akizungumza mbele ya wanahabari

KANDANDA Kocha Benchikha ataka straika mpya Simba

Na Zahoro Juma • 16:30 - 14.01.2024

Hatua hiyo imetokana na kocha huyo kukosa ubingwa wa Mapinduzi Cup baada ya kufungwa bao 1-0 na Mlandege FC

Kocha wa timu ya Simba SC, Abdelhak Benchikha, amesema timu hiyo inahitaji kupata mshambuliaji wa daraja la juu ili iweze kushindana na timu kubwa katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Hayo ameyasema mara baada ya kupokea kichapo cha 1-0 kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi uliofanyika katika Uwanja wa New Amani Complex.

Benchikha amesema timu yake mara tu baada ya kuruhusu bao ilikosa mbinu sahihi na wachezaji bora ambao wanaweza kupiga pasi za mwisho huku pia akitaja nafasi ya ushambuliaji kama tatizo kikisoni hapo.

"Tuliporuhusu bao tulikosa mbinu za kuwafungua wapinzani kwasababu hatuna mtu wa kupiga pasi nzuri za mwisho na mshambuliaji," amesema.

Ameongeza kwa kusema timu kama Simba ambayo inashiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika inatakiwa kuwa na mshambuliaji wa maana.

Simba katika mchezo dhidi ya Mlandege, imewatumia washambuliaji wao, Mosses Phiri ambaye alianza kipindi cha kwanza na kisha akampisha Jean Baleke kipindi cha pili.

Mbali na washambuliaji hao lakini pia kwenye kikosi hicho yupo mshambuliaji na nahodha wao, John Bocco ambaye kwenye mchezo wa fainali hakucheza.

Bao la Mlandege kwenye mchezo huo, limefungwa na mshambuliaji, Joseph Akandwanaho dakika ya 54 kipindi cha pili.

Katika dirisha hili la usajili ambalo linatarajia kufungwa kesho, Simba imefanya ongezeko la wachezaji watatu hadi sasa ambao ni mawinga, Ladack Chasambi na Saleh Karabaka wote kutoka Tanzania lakini pia wameongeza kiungo mkabaji, Babacar Sarr raia wa Senegal.

Simba ina kibarua cha kufuzu kucheza robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika wakiwa wamebakisha mechi mbili dhidi ya Jwaneng Galaxy nyumbani na mechi dhidi ya Asec Mimosa ugenini.

Tags: