Yanga yaleta straika mpya kutoka Ulaya

KANDANDA Yanga yaleta straika mpya kutoka Ulaya

Na Zahoro Juma • 09:40 - 16.01.2024

Nyota huyo ni raia wa Ivory Coast ambaye alikuwa akiichezea Klabu ya Tuzlaspor ya nchini Uturuki

Klabu ya soka ya Yanga, imefunga usajili wake kwa kusajili mshambuliaji raia wa Ivory Coast, Joseph Guede akiwa anatoka katika Klabu ya Tuzlaspor inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini Uturuki.

Kabla ya kwenda Uturuki, mwanzoni mwa msimu huu mchezaji huyo alikuwa akicheza katika timu ya FAR Rabat ambayo alichukuwa nayo ubingwa wa ligi msimu uliopita.

Guede, 29, akiwa FAR Rabat amewahi kwenda kwa mkopo katika timu ya Emirates inayoshiriki Ligi katika nchi ya Falme za Kiarabu (UAE).

Kuingia kwa mshambuliaji huyo pia kumetoa fursa kwa mshambuliaji mwengine wa Yanga, Hafiz Konkoni kutolewa kwa mkopo katika timu ya Dogan Turk Burlig inayoshiriki Ligi ya Cyprus.

Awali Yanga walimsajili Konkoni akiwa kama mbadala wa mshambuliaji wao wa zamani, Fiston Mayele lakini inaonekana mchezaji huyo hakuweza kupenya kwenye kikosi cha kwanza cha Kocha, Miguel Gamondi.

Licha ya timu yake kuwa na wachezaji wengi eneo la ushambuliaji lakini kocha Gamondi hakuacha kusisitiza umuhimu wa kupatiwa mchezaji mpya ambaye atakuwa mfungaji kiongozi ndani ya Yanga.

Hadi hatua hii ambayo Yanga wamefika katika ligi na michuano ya kimataifa, walikuwa wakiwatumia zaidi washambuliaji Clement Mzize na Kennedy Musonda katika mechi nyingi huku kinara wao wa mabao katika Ligi Kuu akiwa ni Stephan Aziz Ki kama ilivyo Pacome Zouzoua katika michuano ya kimataifa.

Kwa ujumla, Yanga katika dirisha hili wamenasa saini za wachezaji watatu ambapo Guede ataungana na Shekhan Ibrahim na Augustine Okrah ambao walitangulia kutangazwa.

Wachezaji ambao wametangazwa kuondona ni Jesus Moloko ambaye ameachwa na Crispin Ngushi ametolewa kwa mkopo Coastal Union ya Tanga kama ilivyo kwa Konkoni ambaye ametolewa kwa mkopo Cyprus.

Tags: