Mwakinyo atwaa ubingwa wa WBO Afrika
Bondia wa ngumu za kulipwa wa nchini Tanzania, Hassan Mwakinyo, amesema yupo tayari kupigana na bondia yeyote wa ndani endapo watapatikana watu wa kuandaa pambano hilo.
Hayo amesema akiwa visiwani Zanzibar kwenye Uwanja wa New Amani Complex mara baada ya kuibuka na ushindi wa TKO ya raundi ya saba dhidi ya Mghana, Elvis Ahorgah.
Ushindi huo ulimuhakikishia Mwakinyo 'Champez' kunyakuwa taji la WBO Afrika.
"Nashukuru kwa ushindi huu, nilipata upinzani mkali kutoka kwa mpinzani wangu lakini nimefanikiwa kumpiga, hii inaonesha ni kwa kiasi gani nipo fiti na nipo tayari kucheza na bondia yeyote wa ndani au wa nje endapo watapatikana waandaaji," amesema.
Kwa muda mrefu kumekuwa na hamu ya wapenzi wa masumbwi nchini kutaka kuona Mwakinyo akifanya pambano na mabondia wazawa hasa Twaha Kiduku kitu ambacho hakijatokea na hivyo kiu imekuwa ni kubwa sana.
Kabla ya kupigana na Ahorgah, bondia Mwakinyo alitarajia kupigana na Mzimbabwe, Enock Msambudzi ambapo haikulezwa wazi hasa ni kipi kilitokea hadi bondia huyo kushindwa kufika nchini.
Katika pambano lingine lililofanyika jijini Tanga, bondia Ibrahim Class ' Ibra Mawe', ameshinda kwa TKO ya raundi ya pili dhidi ya Israel Kammwamba katika pambano ambalo sio la ubingwa lilifonyika uwanjani Mkwakwani.
Class alishinda pambano hilo baada ya kuanza mchezo wake kwa kasi hadi kufikia mpinzani kukosa nafasi ya kujitetea na kuamua kutupa taulo uwanjani.