Licha ya timu ya JKT Queens, kuondolewa katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa Wanawake, timu hiyo imepata dola 100,000 (zaidi ya milioni Tsh200) kutokana na kucheza hatua hiyo ya makundi pekee.
Timu hiyo ilijikuta ikichapwa mabao 4-1 na SC Casablanca ya Morocoo ambayo iliungana na Mamelodi Sundowns Ladies kutinga nusu fainali ya michuano hiyo.
JKT Queens ambayo ilikuwa Kundi A imemaliza ikiwa na alama 3 huku Mamelodi ikiongoza kwa alama 9 ikifuatiwa na Casablanca alama 4 na Atletico Abdijan alama 1 ikishika mkia.
Katika mchezo huo ambao JKT Queens, ilikuwa ikihitaji alama 1 ifuzu, imemaliza ikiwa pungufu baada ya mchezaji wao, Happness Hezron kuoneshwa kadi nyekundu kwa mchezo usiokuwa wa kiungwana.
Kutolewa kwa mchezaji huyo ndipo kukawapa unafuu Casablanca ya kufunga mabao hayo na kufuzu nusu fainali ya michuano hiyo.
Kila timu ambayo imefuzu nusu fainali ya michuano hiyo ina uhakika wa kuondoka na sh. milioni 500 za Kitanzania.
Mabao ya Casablanca yalifungwa na Meryem Hajri, Chaymaa Mourtaji, N'Guessan Nadège Koffi na Adjoa Silviane Kokora huku bao la kufutia macho kwa upande wa JKT likifungwa na Stumai Abdallah.