Klabu ya Soka ya Al Hilal ya Sudan, imekubaliwa na Serikali ya Tanzania kuchezea mechi zao za Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam.
Nchi hiyo imeendelea kuwa kivutio kwa timu nyingi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kuchagua kuutumia uwanja huo sababu ikitajwa kuwa ni ubora na hamasa kwa mashabiki wa soka nchini hapa.
Al Hilal ambao wapo chini ya Kocha, Florent Ibenge, wamepangwa Kundi C pamoja na timu za Esperance de Tunis, Etoile du Sahel na Petro de Luanda.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na klabu hiyo kupitia ukurasa wao wa mtandao wa kijamii wa Instagram, wameishukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwakubalia ombi lao.
Hivi karibuni pia tulishuhudia TP Mazembe ya DR Kongo ambao nao waliutumia uwanja huo katika mechi yao ya michuano ya AFL dhidi ya Esperance de Tunis ya Tunisia.
Katika mchezo huo, Mazembe walipata mwitikio mkubwa kutoka kwa mashabiki wa soka nchini ambao walijitokeza kwa wingi na kushuhudia mechi hiyo.
Al Hilal kwasasa wapo katika wakati mgumu kutumia uwanja wa ardhi ya nyumbani kwao Sudan kutokana na machafuko ya kisiasa yaliyosababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe yanayoendelea tangu yalipoanza Aprili, mwaka huu.