Yanga SC yaingia ushirikiano na Aga Khan

Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said (kushoto), akishukuru na Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma za Afya Agha Khan, Sisawo Konteh baada ya kusaini mkataba

KANDANDA Yanga SC yaingia ushirikiano na Aga Khan

Zahoro Juma • 21:36 - 06.02.2024

Ushirikiano huo utawanufaisha viongozi, wachezaji pamoja na wanachama wa klabu hiyo katika kupata huduma mbalimbali

Klabu ya soka ya Yanga, imetangaza kuingia mkataba wa ushirikiano na taasisi ya kutoa huduma za afya nchini Aga Khan.

Akizungumza wakati wa utiaji saini wa makubaliano hayo, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, ameema ushirikiano waliongia na Hospitali ya Aga Khan utakuwa unalenga katika maeneo matatu.

Ameyataja maeneo hayo kuwa ni kutoa elimu ya afya kwa jamii ambapo Agha Khan pamoja na Yanga watashirikiana katika kusambaza elimu mbalimbali.

Mbali na eneo hilo lakini pia wachezaji na viongozi wa Yanga watakuwa wakipata huduma zao mbalimbali za kiafya katika hospitali ya Agha Khan.

Hersi ametaja eneo la mwisho la ushirikiano kuwa ni upande wa wanachama wa Yanga ambapo kwa kila mwenye kadi hai basi kutakuwa na punguzo maalumu wakati akipatiwa huduma za afya ndani ya hospitali hiyo.

"Leo taasisi kubwa nchini zimekubaliana kufanya kazi kwa pamoja, Yanga kama taasisi namba moja kwa mpira na Agha Khan kama taasisi kubwa katika sekta ya afya," amesema.

"Tunalenga kuweka ushirikiano katika kusambaza elimu, lakini wachezaji pamoja na viongozi watatibiwa hapa na kutakuwa na punguzo maalumu kwa wanachama wenye kadi hai," amemalizia Hersi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma za Afya Agha Khan, Sisawo Konteh, amewataka wanachama wa Yanga na watanzania kwa ujumla kufanya huduma zao katika hospitali hiyo kwakuwa zinagharama nafuu tu kama sehemu nyingine.

Amesema taasisi ya Agha Khan hapa Tanzania ina jumla ya matawi 27 ambayo yamesambaa katika maeneo mbalimbali na huduma zinazopatikana huko ni kama zile ambazo zinapatikana makao makuu.

Yanga ipo katika shamra shamra za kuelekea kilele cha kutimiza miaka 89 ya tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo ambapo imetangazwa kuwa sherehe zake zitafanyika mkoani Mbeya, Februari 11.