Yanga SC kusherekea ‘birthday’ ya miaka 89 Mbeya

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, akizungumza

KANDANDA Yanga SC kusherekea ‘birthday’ ya miaka 89 Mbeya

Zahoro Juma • 16:00 - 05.02.2024

Itafanya sherehe hiyo Jumapili ikiwa ugenini kuumana na Prisons katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu

Uongozi wa Klabu ya Yanga, umesema sherehe za kuadhimisha miaka 89 ya timu hiyo kuzaliwa kwake zitafanyika kitaifa mkoani Mbeya.

Hayo yamezungumzwa na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe mapema leo wakati akizundua wiki ya sherehe hizo jijini Dar es Salaam.

Sherehe za mwaka huu zitafanyika siku hiyo ambayo pia Yanga itakuwa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa Uwanja wa Sokoine.

Kamwe amesema ndani ya wiki hii uongozi wa Yanga utafanya shughuli mbalimbali ikiwemo kusaini mikataba miwili mipya na taasisi tofauti ambayo itakuwa na lengo la kuwanufaisha wanachama.

Mbali na matukio hayo lakini pia wanatarijia kufanya uzinduzi wa makao yao makuu eneo la Mtaa wa Twiga na Jangwani, Kariakoo ikiwa ni baada ya kuzifanyia maboresho kwa kipindi cha hivi karibuni.

"Katika wiki hii sisi kama viongozi tutafanya mambo kadhaa yanayolenga kuwasaidia wanachama wetu wakati tunasherehekea miaka 89 ya kuanzishwa kwa klabu yetu," amesema.

Amewataka wanachama na mashabiki wa Yanga popote walipo nchini kufanya mambo mbalimbali kwenye jamii ikiwemo kufanya usafi na kutoa misaada kwa wahitaji hasa kuchangia damu katika hospitali.

Klabu hiyo ilizaliwa rasmi Februari 11, 1935 na imekuwa na mafanikio makubwa katika soka la Tanzania na Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla wake.