Singida FG yautaka ubingwa Tanzania

KANDANDA Singida FG yautaka ubingwa Tanzania

Zahoro Mlanzi • 21:34 - 11.09.2023

Singida FG ilimaliza nafasi ya nne msimu uliopita baada ya kuzidiwa ujanja na Azam FC, Simba SC na Yanga SC

Timu ya Singida Fountain Gate, imesisitiza malengo yao msimu huu 2023/24 ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Singida FG ilimaliza nafasi ya nne msimu uliopita baada ya kuzidiwa ujanja na Azam FC, Simba SC na Yanga SC ambayo ndio ilitwaa ubingwa kwa mara ya pili mfululizo.

Akizungumza na Pulsesports, Ofisa Habari wa timu hiyo, Hussein Massanza, amesema malengo hayo yanawafanya wakamiwe na timu mbalimbali za ligi hiyo lakini watahakikisha wanafikia malengo.

"Inawezekana baada ya kuweka wazi nia yetu msimu huu, kila timu tutakayokutana nayo inatukamia...ndio maana hata mechi zetu mbili za kwanza hatujapata matokeo mazuri," amesema Massanza.

Singida FG ilitoka suluhu na Tabora United kabla ya kupata matokeo kama hayo mbele ya Prisons.

Amesema timu hizo zina bahati kwakuwa walianza ligi hiyo wakiwa hawana kocha na ndio maana wakapata matokeo hayo lakini kwa hivi sasa watakayekutana naye lazima wamfunge.

"Tulikuwa na Kocha, Hans van Pluijm ambaye kabla ya ligi kuanza aliomba kuondoka...tukamuomba abakie hadi tutakapopata kocha mwingine, tunamshukuru Mungu tumeshapata kocha mpya na ndio maana tunasisitiza malengo yetu yapo pale pale," amesisitiza Massanza.

Singida FG ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kama Singida Big Stars, itashuka uwanjani Jumapili kuumana na Future FC katika mechi ya mkondo wa kwanza kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kabla ya kurudiana mwishoni mwa mwezi huu nchini Misri.

Ilitinga hatua hiyo baada ya kuifunga JKU ya Zanzibar kwa mabao 4-3.