Singida FG yapania makubwa Misri

© Kwa Hisani

KANDANDA Singida FG yapania makubwa Misri

Zahoro Mlanzi • 20:00 - 25.09.2023

Timu hiyo inatarajia kuondoka Alhamisi kwenda kuumana na timu hiyo katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Wachzaji wa timu ya Singida Fountain Gate, wameahidi kujituma kwa hali na mali kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mchezo wao dhidi ya Future ya Misri.

Timu hiyo inatarajia kuondoka Alhamisi kwenda kuumana na timu hiyo katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, mchezo utakaopigwa Oktoba Mosi Uwanja wa Al-Salaam jijini Cairo, Misri.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Singida iliibuka na ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na Mkenya Elvis Rupia.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa mazoezi kujiandaa na mchezo huo, wachezaji hao, wamesema uwezo wa kutinga hatua ya makundi wanao kikubwa wanatakiwa kucheza kwa nidhamu.

Beno Kakolanya ambaye ni kipa wa timu hiyo, amesema licha ya mchezo huo utapigwa ugenini, lakini anaiona nafasi ya timu yao kutinga makundi ya michuano hiyo.

Amesema wenzao Simba na Yanga zimejiweka pazuri, lakini wao ni ngumu kwa kuwa walianzia nyumbani na ushindi mwembamba.

Hata hivyo, kipa huyo amesema ushindi waliopata nyumbani unawapa nguvu ya kutinga makundi na kwamba kila mchezaji atajitolea kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

Pia beki mkongwe, Mkenya Joash Onyango ambaye anaichezea timu hiyo kwa mkopo akitokea Simba SC, amewaomba wachezaji watakaopata nafasi ya kuanza kucheza kwa bidii, kujituma na kwa umakini.

"Hakuna ambacho kinashindikana, kikubwa ni kujitoa tu kwa hali na mali, tunajua tutakuwa ugenini lakini mpira wa sasa una mabadiliko makubwa, haijalishi unacheza wapi muhimu ni kupata matokeo," amesema Onyango.