Simba yafikisha mechi 26 'unbeaten' Ligi Kuu

© Kwa Hisani

KANDANDA Simba yafikisha mechi 26 'unbeaten' Ligi Kuu

Zahoro Mlanzi • 19:36 - 21.09.2023

Ushindi huo, umeifanya Simba kufikisha michezo 26 mfululizo wa ligi hiyo bila kufungwa.

Mabao matatu yaliyofungwa kipindi cha kwanza na Mkongo, Jean Baleke, yameiwezesha timu yake ya Simba SC kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ushindi huo, umeifanya Simba kufikisha michezo 26 mfululizo wa ligi hiyo bila kufungwa.

Mara ya mwisho Simba kufungwa katika ligi hiyo ilikuwa Oktoba 27, ilipopoteza mbele ya Azam FC kwa bao 1-0 lililofungwa na straika, Prince Dube.

Timu hiyo inaisaka rekodi iliyowekwa na Yanga ya kucheza mechi 49 mfululizo bila kupoteza.

Matokeo hayo yaliyopatikana jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, yameifanya Simba kuisogelea Yanga kileleni zote zikiwa na alama 9 ila zinatofautiana kwa mabao huku Mashujaa ikishika nafasi ya tatu kwa alama 7.

Baleke ambaye awali alikuwa na mabao mawili katika ligi hiyo, sasa amefikisha mabao matano na kuwa kinara akimpita Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam ambayo baadaye usiku huu itakuwa uwanjani kuumana na Singida Fountain Gate.

Hata hivyo, Coastal Union ilimaliza mchezo huo ikiwa pungufu baada ya winga wao, Haji Ugando kuoneshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja na Mwamuzi, Ahmed Arajiga baada ya kumchezea vibaya Henock Inonga dakika ya 19.

Inonga amelala chini kwa maumivu makali huku akishikilia goti lake hadi alipokuja kubebwa katika machela na kukimbizwa katika gari ya wagonjwa mahututi kwa matibabu zaidi.

Baleke amefunga bao la kwanza ndani ya dakika 6 za kwanza, akiitendea haki pasi ya Clatous Chama.

Zikapita dakika nne, Baleke akafunga bao la pili baada ya kuunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Mohamed Tshabalala aliyeuwahi mpira uliotemwa na Kipa, Robert Chuma aliyepangua shuti la Saido Ntibazonkiza.

Simba imeendelea kutawala mchezo na kuipa wakati mgumu Coastal hata hivyo ikajikuta inacheza pungufu baada ya Ugando kutolewa kwa kadi nyekundu kitu kilichomuumiza nahodha wake, Ibrahim Ajibu ambaye alionekana kutaka kulia.

Simba imeongeza presha kwa Coastal na dakika ya 37, Luis Miquissone, aliangushwa ndani ya eneo la hatari na Dennis Modzaka na kuwa penalti iliyowekwa kimiani na Baleke.

Hata hivyo kipindi cha pili, Coastal imerudi na nguvu mpya na kuonesha ushindani ila mastraika wake walikosa umakini kukwamisha mipira wavuni.