Yanga ni kicheko Ligi Kuu Tanzania Bara

Kwa Hisani

KANDANDA Yanga ni kicheko Ligi Kuu Tanzania Bara

Zahoro Mlanzi • 19:34 - 21.09.2023

Ushindi huo, umeifanya Yanga kufikisha alama 9 kutokana na kushinda michezo yake mitatu ya kwanza.

Bao pekee lililofungwa na kiungo, Mudathir Yahya dakika ya 88, limeiwezesha timu ya Yanga kuendeleza wimbi la ushindi wa asilimia 100 katika Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo.

Mudathir aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Pacome Zoazoua, alifunga bao hilo usiku huu uwanjani Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam baada ya kuitendea haki pasi iliyopigwa na beki wa kulia, Kouassi Attohoula.

Ushindi huo, umeifanya Yanga kufikisha alama 9 kutokana na kushinda michezo yake mitatu ya kwanza ikifuatiwa na Mashujaa FC yenye alama 7 huku Simba SC ambayo kesho itacheza na Coastal ya Tanga ikishika nafasi ya tatu ikiwa na alama 6.

Wachezaji na mashabiki wa Namungo ambao leo asubuhi wamewapoteza wenzao wanne katika ajali ya gari, hadi kufikia dakika hizo waliamini wataondoka na alama moja ugenini.

Namungo ambayo inatoka Kusini mwa Tanzania, muda mwingi imecheza kwa kupaki basi kwa kutumia mfumo wa 5-3-2 na kuwapa wakati mgumu wachezaji wa Yanga kuipita safu yao ya ulinzi ambapo walitumia mfumo wa 4-2-3-1.

Hadi dakika 45 za kwanza zikimalizika, timu hizo zimetoka suluhu huku Yanga ikitengeneza nafasi tatu za wazi hata hivyo Stephano Aziz KI na Pacome walishindwa kuzitendea haki.

Shambulizi pekee ambalo Namungo itajutia ni walilofanya dakika ya 48 ambapo Emmanuel Charles akiwa katika nafasi ya kufunga alipiga shuti lililotoka pembeni ya goli akiwahi mpira mrefu uliopigwa na Shiza Kichuya.

Yanga iliendelea kutengeneza nafasi lakini ilionekana kama hawana bahati katika siku ya leo kwani mashambilizi mengi yalikuwa yakitua mikononi mwa Kipa wa Namungo, Deogratius Munishi 'Dida'.

Ligi hiyo itaendelea kesho kwa kuchezwa mechi mbili kati ya Simba SC itakayaoikaribisha Coastal mchezo utakaopigwa saa 10 jioni Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na kufuatiwa na mechi ya Azam FC itakayoumana na Singida Fountain Gate saa 1 usiku.