Yanga SC yamtoa Ngushi kwa mkopo Coastal Union

Straika wa Yanga, Crispin Ngushi, akiwa katika majukumu yake uwanjani

KANDANDA Yanga SC yamtoa Ngushi kwa mkopo Coastal Union

Zahoro Juma • 21:22 - 13.01.2024

Straika huyo ambaye alisajiliwa kutoka Mbeya Kwanza, ameshindwa kuendana na kasi ya timu hiyo

Klabu ya Soka ya Yanga, imempeleka mshambuliaji wake, Crispin Ngushi kucheza kwa mkopo ndani ya Coastal Union ya Tanga hadi mwisho wa msimu.

Huyo anakuwa mchezaji wa kwanza kwa timu hiyo kuondolewa kikosini ikipita siku moja tangu Kocha, Miguel Gamondi kuweka wazi kuwa atapitisha fagio.

Kwa mujibu wa taarifa ya Yanga kupitia mtandao wao wa X, imeeleza: "Mchezaji wetu Crispin Ngushi anajiunga na Coastal Union kwa mkopo mpaka mwisho wa msimu,".

Ngushi alijiunga na Yanga dirisha dogo Januari 8, mwaka 2022 akitokea Mbeya Kwanza lakini ameshindwa kuendana na kasi ya timu hiyo.

Kwa nyakati tofauti msimu uliopita akiwa chini ya Kocha, Mtunisia Nasreedin Nabi, alipewa nafasi ya kutosha hata hivyo alishindwa kumshawishi kocha huyo.

Hata alivyokuja Gamondi, mwanzoni msimu huu licha ya kumpa nafasi katika baadhi ya mechi za Ligi Kuu Bara na kwa kiasi kikubwa katika Mapinduzi Cup, bado hali imekuwa vile vile.

Katika michuano ya Mapinduzi Cup ambayo fainali yake inachezwa leo saa 2:15 usiku kati ya Mlandege FC na Simba SC, Ngushi alifunga mabao mawili na kutengeneza moja.