VAR kutumika Ligi Kuu Tanzania Bara

© Kwa Hisani

KANDANDA VAR kutumika Ligi Kuu Tanzania Bara

Zahoro Mlanzi • 07:40 - 19.10.2023

Licha ya kukiri kuwa teknolojia ya VAR ni ghali lakini Mwana FA, amesema ni muhimu kufikia huko sambamba na kuboresha maslahi ya waamuzi nchini.

Naibu Waziri wa Sanaa,Utamaduni na Michezo, Khamis Mwinjuma 'Mwana FA', amesema ili kupunguza makosa ya waamuzi katika Ligi ya Tanzania Bara ni lazima kuja na njia mbadala ikiwemo kufunga video za usaidizi (VAR).

Licha ya kukiri kuwa teknolojia ya VAR ni ghali lakini Mwana FA, amesema ni muhimu kufikia huko sambamba na kuboresha maslahi ya waamuzi nchini.

Hayo ameyaongea mubashara wakati akifanya mahojiano na Wasafi FM jijini Dar es Salaam.

Mwana FA amesema yeye kwa muda mrefu amekuwa ni mtu wa mpira na pia amekuwa akishuhudia makosa mengi ya waamuzi ambapo amedai kuwa yapo ambayo yanaonekana ni ya kibinadamu lakini yapo ya makusudi.

"Kama mnavyonijua mimi ni mtu wa mpira, nimekuwa nikishuhudia makosa mengi ya kiuwamuzi ambapo yamegawanyika mara mbili, yapo yakibinadamu lakini pia yapo ya makusudi," amesema.

"Ili kujirekebisha katika eneo hilo inatupasa kuingia katika mfumo wa kisasa wa VAR ili kuyatoa makosa ya bahati mbaya, lakini pia tuboreshe maslahi kwa ajili ya kuondoka makosa ya makusudi," amesema.

Aidha akijibu swali kuhusu kuzorota kwa hamasa kwa upande wa timu ya Taifa 'Taifa Stars' kwa siku za hivi karibuni licha ya kufuzu Afcon, Mwana FA alisema huo ni mkakati wa makusudi uliofanywa baina ya TFF na serikali ili timu iweze kufanya vizuri.

"Baada ya kufungwa na Uganda hapa nyumbani tulikaa na kubaini kuwa hamasa kubwa inayofanywa nje ya uwanja huwa inawaongezea presha wachezaji hivyo tulikubaliana kuwa kuelekea michezo muhimu dhidi ya Niger na Algeria tulikaa kimya ili timu ifanye vizuri," amesema.