Al Ahly yatua Dar kuumana na Simba SC

© Kwa Hisani

KANDANDA Al Ahly yatua Dar kuumana na Simba SC

Zahoro Mlanzi • 21:38 - 18.10.2023

Al Ahly wakiongozwa na Kocha Mkuu, Marcel Koller, wameingia wakiwa na wachezaji wao wote waandamizi akiwemo nahodha, Mohamed El Shenawy.

Kikosi kamili cha timu ya Al Ahly ya Misri, ambao ni wapinzani wa Simba kwenye michuano ya AFL, tayari kimetua nchini Tanzania kwa ajili mchezo huo ambao unatarajiwa kupigwa Ijumaa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Al Ahly wakiongozwa na Kocha Mkuu, Marcel Koller, wameingia wakiwa na wachezaji wao wote waandamizi akiwemo nahodha, Mohamed El Shenawy ambaye hii si mara yake ya kwanza kuja Tanzania.

Mbali na Shenawy lakini pia Al Ahly wameambatana na wachezaji wao nyota kama Percy Tau, Aliou Dieng na Anthony Moderate aliyesajiliwa msimu huu kutoka Borrusia Dortmund ya Ujerumani na wachezaji hao wanatarajiwa kuwa mwiba dhidi ya Simba kwenye mchezo huo.

Mlinzi wa kutumainiwa wa kikosi hicho, Ali Maaloul yeye ataungana na timu hiyo hapa Tanzania akiwa amesafiri pekee yake kutokea Japan ambapo alikuwa na mchezo wa kirafiki baina ya timu yake ya Taifa ya Tunisia dhidi ya Japan mchezo uliochezwa Jumatatu.

Simba ndio wenyeji kwenye mchezo huo wa ufunguzi wa michuano hii mipya lakini mara baada ya mchezo huo wa Ijumaa watalazimika kusafiri kwenda Misri kwa ajili ya mchezo wa marudiano ambao utachezwa Oktoba 24 na mshindi wa jumla baada ya mechi mbili atasonga mbele kwenye hatua ya nusu fainali.

Mara ya mwisho kwa klabu hizo kukutana kwenye Uwanja wa Mkapa, ilikuwa ni Februari 2021 ambapo bao la Luis Miquisonne liliipa ushindi wa 1-0 Simba kwenye mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.