Onyango aachwa safari Misri

© Kwa Hisani

KANDANDA Onyango aachwa safari Misri

Zahoro Mlanzi • 21:00 - 26.09.2023

Singida FG inakwenda kucheza mechi yao ya mkondo wa pili ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Future FC.

kikosi cha wachezaji 23 wa timu ya Singida Fountain Gate, kinaondoka jioni ya leo kwenda Misri, Beki mkongwe wa timu hiyo, Joash Onyango, amebakia nchini.

Timu hiyo inakwenda kucheza mechi yao ya mkondo wa pili ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Future FC ya nchini Misri, utakaopigwa Oktoba Mosi kwenye Uwanja wa Al Salam jijini Cairo.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Azam Complex, Dar es Salam, Singida iliibuka na ushindi wa bao 1-0, likifungwa na Mkenya, Elvis Rupia.

Akizungumza na Pulse Sports, Ofisa Habari wa timu hiyo, Hussein Massanza, amesema baada ya kufanya maandalizi chini ya benchi lao la ufundi, sasa wapo tayari kwenda kumalizia kazi waliyoianza.

"Hatutaweza kuondoka na wachezaji wote tuliowasajili, baada ya mazoezi hayo benchi la ufundi limeteua majina ya wachezaji 23 ambao wanaamini watakwenda kupambana," amesema Massanza na kuongeza.

"Mwalimu na wachezaji wanajua umuhimu wa mchezo huo na dhamira yao ni kuona wanatinga hatua ya makundi ya michuano hii."

Amesema wanaenda Misri wakijua wanakwenda kupambana na kuipeperusha vyema Bendera ya Taifa kwa kupata matokeo mazuri.

"Tumechukua wachezaji hawa 23 ili kuwa na wasaidizi wa kutosha, kucheza na waarabu ugenini si jambo dogo, watabadilika sana hawatakuwa wale tuliokutana nao hapa," amesisitiza Massanza.

Amewataja wachezaji wanaoondoka ni makipa, Beno Kakolanya, Ibrahim Rashid na Benedict Haule, mabeki ni Laurian Makame, Biemes Carno, Hamad Waziri, Kelvin Kijiri, Yahya Mbegu na Gadiel Michael.

Viungo ni Moroce Chukwu, Aziz Andambwile, Yusuph Kagoma, Deus Kaseke, Dickson Ambundo, Duke Abuya, Bruno Gomes na Marouf Tchakei huku mastraika ni Meddie Kagere, Rupia, Francy Kazadi na Thomas Ulimwengu.