Yanga yapata pigo mechi ya CAF

© Kwa Hisani

KANDANDA Yanga yapata pigo mechi ya CAF

Zahoro Mlanzi • 20:53 - 25.09.2023

Beki hiyo wa kushoto, amepata maumivu hayo baada ya kuchezewa vibaya na Hashim Manyanya na moja kwa moja kutolewa nje ya uwanja.

Timu ya Yanga, imepata pigo baada ya beki wao wa kimataifa wa DR Congo, Lomalisa Mutambala, kutakiwa kukaa nje ya uwanja kwa siku tano baada ya kuumia paja wakati wa mchezo wao dhidi ya Namungo FC.

Beki hiyo wa kushoto, amepata maumivu hayo baada ya kuchezewa vibaya na Hashim Manyanya na moja kwa moja kutolewa nje ya uwanja.

Lomalisa ambaye amekuwa na wakati mzuri tangu asajiliwe na timu hiyo msimu uliopita, hatokuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kitakachorudiana na Al-Merreikh ya Sudan katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Daktari wa timu hiyo, Mosses Itutu, amesema amepata majeraha katika paja na kuchubuka ingawaje hajaamia sana.

"Lomalisa tulijaribu kumpa matibabu wakati mchezo ukiendelea lakini alishindwa, hivyo tukaona tumpe muda wa kupumzika ili aweze kupona vizuri na atakuwa nje kwa siku tano hadi saba," amesema Itutu.

Hata hivyo, wakati wenzake wakiwa mazoezini leo asubuhi kambini Avic Town Kigamboni, Dar es Salam, kujiandaa na Al-Merreikh, beki huyo alifika na kukaa nje ya uwanja akiangalia kinachoendelea uwanjani.

"Nilitaka kuendelea na mchezo lakini nimeshindwa kutokana na kuchezewa ile rafu, ndio mambo ya uwanjani yanavyokuwa," amesema Lomalisa.

Ameulizwa kwanini alitoka uwanjani akiwa analia, Lomalisa amejibu:" Ni maumivu niliyokuwa nikiyasikia, lakini pia wakati natoka timu yetu ilikuwa haijafunga bao, nikawa na mawazo mawili mawili.

Katika mchezo huo uliopigwa Jumatano wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Mudathir Yahya.