Gamondi: Yanga inashinda lakini haichezi vizuri

LIGI KUU Gamondi: Yanga inashinda lakini haichezi vizuri

Zahoro Juma • 19:36 - 09.02.2024

Kauli hiyo imekujaa baada ya kuiongoza timu hiyo kushinda mechi mbili na sare moja

Kocha wa timu ya Yanga SC, Miguel Gamondi, amesema kwasasa kitu muhimu kwake ni alama tatu katika kila mchezo.

Hayo amesema mara baada ya kumalizika kwa mechi ya Ligi Kuu Bara ambapo timu yake iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa FC katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, iliwalazimu Yanga kusubiri tena hadi dakika za mwishoni ili kufunga bao la ushindi kupitia kwa kiungo wao, Mudathir Yahaya.

Mara baada ya mchezo huo, Gamondi amesema timu yake kwasasa haichezi kama alivyotarajia lakini kitu muhimu kwake ni kuvuna alama tatu.

"Kwasasa hatupo katika hali nzuri ya kiushindani kama tulivyokuwa awali, hata hivyo muhimu zaidi tunavuna alama tatu," amesema.

Tangu kurejea kwa ligi hiyo, Yanga imecheza mechi tatu ambapo walianza kwa kulazimishwa suluhu na Kagera Sugar ugenini.

Mara baada ya mchezo huo, wakacheza mechi mbili dhidi ya Dodoma Jiji na Mashujaa ambapo mechi zote hizo walipata mabao ya ushindi kwenye dakika tano za mwisho.

Yanga sasa inajiandaa kwenda kukabiliana na Tanzania Prisons ya mkoani Mbeya mechi ambayo itachezwa kesho Uwanja wa Sokoine.