Gamondi: Ni bahati kutofungwa nyingi na APR

KANDANDA Gamondi: Ni bahati kutofungwa nyingi na APR

Zahoro Mlanzi • 19:38 - 08.01.2024

Kocha huyo wa Yanga, amejikuta katika wakati mgumu kuondolewa katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Mapinduzi Cup

Kocha wa timu ya Yanga SC, Miguel Gamondi, amesema ingeweza kuwa maafa zaidi kwa timu yake kama APR wangeweza kutulia na kutumia nafasi walizopata kipindi cha pili.

Hayo amesema wakati akielezea mchezo wa robo fainali ya michuano ya Mapinduzi Cup ambapo Yanga ilitupwa nje kwa kufungwa 3-1 na timu ya APR kutoka Rwanda.

Mbali na hayo lakini pia Gamondi hakusita kuwakumbuka wachezaji wake 14 wa kikosi cha kwanza ambao amewakosa katika michuano hiyo kwasababu mbalimbali.

Yanga katika mchezo dhidi ya APR, ilitangulia kwa kufunga bao la mapema kwenye kipindi cha kwanza kupitia kwa winga wao Jesus Moloko.

Hata hivyo wageni waalikwa kwenye michuano hiyo, APR walichomoa bao hilo zikiwa zimesalia sekunde kabla ya timu kwenda mapumziko kupitia kwa Soulei Sanda.

Kipindi cha pili kilikuwa kichungu zaidi kwa Yanga kwani APR walikuja kama mbogo aliyejeruhiwa na katika dakika ya 47 tu walipata penati ambayo ilifungwa na Mbaoma Victor.

Mara baada ya bao hilo Yanga, ilionekana kukatika na kuwapa nafasi zaidi APR kuliandama lango lao kwa mashambulizi ya kushtukiza ambayo yalionekana yangeweza kuwa mabao kama wangekuwa makini.

Bao la tatu kwa APR lilifungwa na Sharif Shaiboub.

"Tulipoteza utulivu baada ya kuruhusu bao la pili, wachezaji wangu walipoteza umakini na kusababisha kuacha nafasi kubwa kwa wapinzani kuushika mchezo, kama wangekuwa makini basi mechi kama hizi huwa zinaisha na mabao mengi zaidi," amesema Gamondi.

Hata hivyo, licha ya kupoteza mchezo huo lakini Kocha Gamondi amewasifu vijana aliowapa nafasi kwa kusema wameonesha utayari wao katika kugombea nafasi za kikosi cha kwanza.

Amesema amepata mwanga kuhusu uwezo wa wachezaji hao ambao wengi wanacheza katika timu ya vijana na kuahidi ataendelea kuwalea ili waje kuwa na msaada baadaye.

"Katika michuano hii imekuwa ni ya mafanikio zaidi kwa vijana wetu na wachezaji ambao walikuwa hawana nafasi ya mara kwa mara kikosini, nimepata picha ya kikosi na tupo katika njia nzuri," amesema.