Wanachama wa Simba SC wapitisha bajeti ya sh. bilioni 25

Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu, akizungumza katika mkutano huo

KANDANDA Wanachama wa Simba SC wapitisha bajeti ya sh. bilioni 25

Na Zahoro Juma • 19:00 - 21.01.2024

Uamuzi huo umefikiwa katika Mkutano Mkuu wa kila mwaka wa wanachama wa klabu hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam

Klabu ya Simba, imepanga kutumia sh. bilioni 25 katika masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwemo usajili wa wachezaji na ujenzi wa miundombinu ya klabu.

Hayo amesema Mhasibu Mkuu wa klabu hiyo, Seleman Kahumbu wakati akitoa taarifa za fedha kwa wanachama waliohudhuria Mkutano Mkuu uliofanyika Dar es Salaam katika Ukumbi wa Kimataifa Mwalimu Julius Nyerere.

Akifafanua taarifa hiyo, Kahumbu, amesema klabu imepanga kukusanya sh. bilioni 25.9 lakini wanatarajia kutumia sh. bilioni 25.4 hivyo watabaki na zaidi ya sh. milioni 500 kama faida kwenye akaunti.

Aidha amesema msimu uliopita klabu ilipanga kutumia sh. bilioni 12 lakini wakatumia kiasi cha sh. bilioni 15.

Kahumbu alisema katika kujazia fedha ambazo zilipungua katika bajeti hiyo, Mfadhili na Rais wa Heshima wa klabu hiyo, Mohemed Dewji ‘Mo Dewji’, alichangia sh. bilioni 2.4.

Wakati huo huo, wanachama wa Simba, wamekubaliana kupitisha rasimu ya katiba mpya inayoruhusu mabadiliko ya uendeshaji lakini wamekataa kipengele namba 19 kinachohusu 'wanaotakiwa kuhudhuria mkutano mkuu'.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Mabadiliko ya Katiba, Hussein Kitta, wamependekeza kuwe na uwakilishi wa wanachama wanaohudhuria Mkutano Mkuu wa kila mwaka kitu ambacho wajumbe wa mkutano wamepinga.

"Tulipendekeza kwamba kutakuwa na uwakilishi katika mkutano mkuu lakini wajumbe wamepinga kipengele hicho na hivyo tunarudi kwa ajili ya kubadilisha ili tuendelee na mambo mengine," amesema Kitta.

Awali akizungumza mbele ya wanachama katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, amewataka wanachama kushikamana katika kipindi hiki ambacho timu ipo katika mchakato wa mabadaliko ili kuleta wawekezaji.

"Hatupaswi kubeza mabadiliko wala uwekazaji kwasababu vyote ni vitu muhimu ndani ya klabu yetu, mfano kabla ya kuanza michakato hii timu ilikuwa inaingiza mapato ya sh. biloni 1.6 kwa mwaka lakini sasa hivi tunaingiza sh. bilioni 6.9 kwa mwaka," amesema.

Pia Mangungu alitolea ufafanuzi kuhusu fedha ambazo mashabiki wa Simba walichanga ili kufanya ujenzi wa uwanja wao binafsi ambapo alisema fedha zile zilitumika kujengea uzio wa uwanja wao wa mazoezi uliopo Bunju, Dar es Salaam.

Tags: