Singida Fountain Gate yatambulisha rasmi mrithi wa Hans van der Pluijm

FOOTBALL Singida Fountain Gate yatambulisha rasmi mrithi wa Hans van der Pluijm

Abigael Wafula 18:53 - 01.09.2023

Kocha huyo mpya ana uzoefu na soka la Afrika kwa miaka mingi na amewahi kufundisha klabu zaidi ya 10 barani Afrika.

Klabu ya Singida Fountain Gate, imemtambulisha Mjerumani, Ernst Middendorp,64, kuwa kocha wao mpya akichukua nafasi ya Mholanzi, Hans van ser Pluijm aliyejiuzulu wiki iliyopita.

Middendorp ana uzoefu na soka la Afrika kwa miaka mingi na amewahi kufundisha klabu zaidi ya 10 barani Afrika kama Kaizer Chiefs, Maritzburg United, Swallows, Bloemfountein, Chippa United vyote vya Afrika Kusini, Saint George ya Ethiopia, Asante Kotoko na Hearts of Oak za Ghana.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na klabu hiyo ilieleza:"Tuna furaha kumtangaza Kocha, Ernst Middendorp raia wa Ujerumani kuwa kocha wetu mpya.

Baada ya kutambulishwa ndani ya kikosi hicho, Middendorp, alisema  anatambua kazi haitakuwa nyepesi lakini muhimu kushirikiana.

“Ninatambua kuhusu Ligi ya Tanzania na ushindani wake ulivyo mkubwa hivyo ni muda wa kufanya kazi kwa umakini kufikia mafanikio." 

Kabla ya kuwa kocha, Middendorp alianza kama mchezaji kwenye Klabu ya SG Freren kati ya 1977 na 1981, kabla ya kwenda TuS Lingen katí ya 1981 na 1982, baadaye VfB Rheine katí ya 1982 na 1985 na VfB Alstätte katí ya 1985 na 1987 na amefundisha timu mbalimbali za Ulaya.

Kocha huyo kibarua chake cha kwanza ni kuhakikisha Singida FG inatinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya hivi karibuni kufuzu raundi ya kwanza ya michuano hiyo na itaumana na Future FC ya Misri.

Singida FG imefanya usajili wa nguvu msimu huu kwa kukusanya nyota mbalimbali wa Afrika akiwemo kiungo mshambuliaji, Mkenya Duke Abuya ambaye hivi karibuni ameitwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Kenya ' Harambee Stars'.

Tags: