Simba yaingia kambini kuiwinda JKT Tanzania

Kocha wa Makipa wa timu ya Simba SC, Daniel Cadema, akimfanyisha mazoezi Kipa, Aishi Manula

KANDANDA Simba yaingia kambini kuiwinda JKT Tanzania

Na Zahoro Juma • 20:18 - 14.02.2024

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuyo badala ya Azam Complex kama ilivyotangazwa hapo awali

Kikosi cha timu ya Simba SC kimetua Dar es Salaam na mara moja kimeanza maandalizi kuelekea mchezo wao wa kesho dhidi ya timu ya JKT Tanzania.

Mchezo huo utakuwa ni wa kufunga duru la kwanza kwa timu zote mbili ambapo hadi sasa zimecheza michezo 14 kila mmoja.

Simba mara baada ya kucheza mechi nne mfululizo wakiwa mikoa ya Kanda ya Ziwa, hatimaye imerejea wakiwa na kikosi kamili na wachezaji walipewa siku moja ya mapumziko.

Hata hivyo, wachezaji wote wamekusanyika leo mbele ya Kocha Mkuu Abdelhak Benchikha na maandalizi ya kuwakabili JKT yameanza wakiwa katika Uwanja wao wa mazoezi wa Mo Bunju Arena.

Akizungumza na Pulsesports, Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema lengo la timu yao ni kumaliza mzunguko wa kwanza kwa ushindi kwenye mechi yao ya mwisho.

“Hii ni mechi yetu ya mwisho katika mzunguko wa kwanza, lengo letu ni kumaliza kwa ushindi ili tunapoanza mzunguko wa pili tuwe katika hali nzuri,” amesema.

Simba inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi nyuma ya vinara Yanga, hii ni baada ya kuibuka na ushindi katika mchezo wao waliocheza Jumatatu dhidi ya Geita Gold ambapo walishinda bao 1-0.

Katika kikosi cha Simba wanamkosa mchezaji mmoja tu Henock Inonga ambaye alikuwa akishiriki Afcon na timu yake ya DR Congo na alifika hadi mwisho wa michuano hiyo ambapo walicheza mechi ya mshindi wa tatu.

Hata hivyo muda wowote kuanzia leo mchezaji huyo atajiunga na wachezaji wenzake baada ya kupata mapumziko ya siku kadhaa.

Tags: