Saido, Phiri wairudisha Simba SC kileleni

© Kwa Hisani

KANDANDA Saido, Phiri wairudisha Simba SC kileleni

Zahoro Mlanzi • 22:00 - 08.10.2023

Simba SC wamerudi kileleni Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Singida Fountain Gate.

Timu ya Simba SC, imerejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi mabao 2-1 mbele ya wenyeji Singida Fountain Gate uwanjani Liti, Singida.

Huo ni ushindi wa tamo mfululizo kwa Simba katika ligi hiyo ambao umeifanya kujikusanyia alama 15 na kurejea kileleni ikifuatiwa na Azam FC yenye alama 13 na Yanga alama 12 huku Singida ikibaki nafasi ya tisa kwa alama 5.

Mabao ya Simba katika mchezo huo, yamefungwa na Mrundi Saido Ntibazonkiza na Mzambia Mosses Phiri huku bao pekee la Singida likifungwa na Deus Kaseke.

Katika mchezo huo umekuwa na ushindani mkubwa kwa kila timu kutengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini hazikuwa makini katika kukwamisha mpira wavuni hata hivyo mwisho wa sik Simba ilinufaika na kupata ushindi huo.

Zikapita sekunde 58, tangu Mwamuzi Tatu Malogo kupuliza kipyenga cha kuanza mchezo, straika Mkenya, Elvis Rupia wa Singida, nusura afunge bao la mapema zaidi baada ya kuuwahi mpira mrefu uliopigwa na Duke Abuya na kuingia nao eneo la hatari hata hivyo, Kipa Ally Katoro alitokea na kumnyima uhuru wa kupiga na kujikuta shuti lake likitoka pembeni ya goli.

Simba imejibu shambulizi hilo dakika ya 17, kupitia kwa Kibu Denis ambaye ameingia na mpira ndani ya 18 na kupiga shuti lililopangiliwa na Kipa, Beno Kakolanya na mabeki kuondosha hatari.

Dakika ya 25, Saido amewainua mashabiki wa Simba kwa kufunga bao la kwanza kwa shuti kali nje ya eneo la hatari huku Kakolanya akiruka bila mafanikio baada ya kupokea pasi ya Kibu.

Kaseke ameingia badala ya Bruno Gomes, ameisawazishia Singida zikipita dakika 5 tangu kuanza kwa kipindi cha pili, baada ya Abuya kufanya kazi nzuri ya kumpiga chenga Kennedy Juma na kumpasia Rupia aliyemuwekea katika nafasi nzuri mfungaji kufunga.

Zikiwa zimebaki dakika ya nane kabla ya kipyenga cha mwisho kupulizwa, Phiri amefunga bao la pili akipokea pasi nzuri ya Luis Miquissone na kuifanya Simba kuibuka na ushindi huo.

Katika mchezo mwingine uliopigwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya, wenyeji Tanzania Prisons, imeibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mtibwa Sugar.

Simba kwa sasa haitacheza mchezo wowote wa ligi hadi imalizane na Al Ahly ya Misri katika michuano mipya ya Arican Super League ambapo itacheza nayo Oktoba 20 na marudiano baada ya siku nne nchini Misri.