Rupia ang'ara Singida FG ikitinga nusu fainali Mapinduzi Cup

KANDANDA Rupia ang'ara Singida FG ikitinga nusu fainali Mapinduzi Cup

Zahoro Mlanzi • 20:49 - 08.01.2024

Katika mchezo huo, amefunga bao na kutoa asisti ya bao la ushindi lililoiwezesha timu yake kutinga hatua hiyo.

Straika wa kimataifa wa Kenya, Elvis Rupia, ameibuka shujaa kwa kuisaidia timu yake ya Singida Fountain Gate kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa robo fainali ya Mapinduzi Cup.

Nyota huyo akicheza msimu wake wa kwanza ndani ya timu hiyo, amehusika katika mabao yote akifunga bao la kusawazisha na kisha kutoa asisti ya bao la ushindi kwa Habibu Kyombo.

Rupia hilo ni bao lake la nne katika michuano hiyo akiwiana na Allasane Diao wa Azam FC ambaye katika mchezo huo ndiye aliyefunga bao pekee kwa timu yake.

Hiyo ni mara ya pili mfululizo kwa Azam kutolewa na Singida FG katika michuano hiyo ambapo mwaka jana pia kwenye hatua ya nusu fainali walikubali kichapo cha mabao 4-1.

Katika mchezo huo wa robo fainali uliofanyika Uwanja wa New Amani Complex, visiwani Zanzibar, Azam ndio ilianza kufunga bao kupitia kwa Diao kwenye dakika za majeruhi za kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili, Singida FG ilikuja wakiwa wamejipanga vizuri zaidi na kusawazisha bao kupitia kwa Rupia akimalizia mpira wa krosi uliopigwa na Kyombo.

Bao la ushindi kwa Singida FG, lilifungwa na Kyombo kwa kichwa akiunganisha krosi uliyopigwa na Rupia na baada ya filimbi ya mwisho Kyombo alitangazwa kuwa Mchezaji Bora wa mechi na kuzawadiwa kitita cha shilingi 750,000 na Shirika la Bima la Taifa (NIC).

Singida FG inavuka kucheza nusu fainali ya michuano hii kwa mara ya pili mfululizo huku wakiwa wameshiriki kwa mara ya pili tangu walipopanda daraja.

Kampeni yao msimu uliopita iliwafikisha hadi fainali ambapo walipoteza mchezo mbele ya Mlandege kwa kipigo cha 2-0.

Timu hiyo imeungana na timu za APR na Mlandege katika hatua ya nusu fainali.