Kocha wa Taifa Stars aipania Niger kufuzu Kombe la Dunia 2026

©TFF

KANDANDA Kocha wa Taifa Stars aipania Niger kufuzu Kombe la Dunia 2026

Na Zahoro Mlanzi • 18:47 - 15.11.2023

Stars itaondoka kwa Ndege maalumu ambayo imetolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuwapeleka kwenye mchezo huo na kuwarudisha

Kocha wa timu ya Soka ya Tanzania 'Taifa Stars', Adel Amrouche, ametamba kikosi chake kipo tayari kuumana na Niger katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia 2026.

Timu hiyo inatarajiwa kuondoka kesho kwenda Morocco ambapo mchezo huo ndipo utakapopigwa Novemba 18.

Stars itaondoka kwa Ndege maalumu ambayo ilitolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuwapeleka kwenye mchezo huo na kuwarudisha.

Akizungumzia maandalizi na kambi kwa ujumla, Kocha Amrouche, amesema wachezaji wake asilimia kubwa walikuja wakiwa tayari kwa mchezo huo lakini wapo baadhi ambao hawakuwa sawa hata hivyo kama benchi la ufundi watajitahidi kuunganisha kikosi.

Amrouche amesema michezo iliyokuwa mbele yao yote ni migumu lakini wanajitahidi kusuka mipango ambayo itawapa manufaa uwanjani.

"Michezo yote miwili sio mirahisi lakini ni kazi yetu sisi benchi la ufundi kuhakikisha timu inafanya vizuri," amesema.

Kwa upande wake, Mchezaji mwandamizi ndani ya kikosi hicho, Kiungo Himid Mao anayecheza Klabu ya Ghazl El Mahalla ya nchini Misri, amesema mchezo dhidi ya Niger utakuwa ni mgumu hasa ukizingatia walishakutana na timu hiyo wakati wa kuwania kufuzu Afcon.

Stars inakabiliwa na mchezo mwingine wa michuano hiyo Novemba 21 nyumbani dhidi ya Morocco.

Tags: