Kiungo wa Simba SC kuikosa Power Dynamos

KANDANDA Kiungo wa Simba SC kuikosa Power Dynamos

Festus Chuma • Zahoro Mlanzi • 21:00 - 13.09.2023

Kiungo wa Simba SC hatosafiri na timu kwenda Zambia kwa sababu ya kuumia goti. Timu itacheza na Power Dynamos Jumamosi.

Kiungo wa Simba SC hatosafiri na klabu hicho kwenda Zambia kutokana na jeraha la goti. Simba itamenyana na Power Dynamos Jumamosi.

Kiungo wa kimataifa wa Ivory Coast na timu ya Simba SC, Aubin Kramo, hatosafiri na timu hiyo kwenda Zambia kutokana na kuumia goti.

Kikosi hicho kinatarajia kuanza safari kesho kwenda kuumana na Power Dynamos katika mchezo wa mkondo wa kwanza hatua ya awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wakati kikosi kikiondoka kesho kwa ndege, mashabiki na wanachama wa timu hiyo, wenyewe waling’oa safari yao leo saa 12 jioni wakiwa katika mabasi mawili makubwa.

Akizungumza na Pulsesports, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Ahmed Ally, amesema Kramo aliumia goti katika mchezo wao dhidi ya Ngome FC kisa kilichosababisha kushindwa kufanya mazoezi ya mwisho ya kujiandaa kwa mchezo huo.

"Mustakabali wake utajulikana leo baada ya kupata majibu ya vipimo, aliumia goti la mguu ule ule aliokuwa akisumbuliwa nao, hapa tutajua ni aina gani ya matibabu anatakiwa kufanyiwa," amesema Ally.

Amesema kutokana na hali hiyo ni wazi hatojumuika na kikosi kitakachosafiri kwenda Zambia, atabaki Dar es Salaam kuangalia jinsi gani atapata tiba iliyo bora zaidi.

Kramo tangu asajiliwe na Simba hivi karibuni akitokea Asec Mimosas, amekuwa katika wakati mgumu kwani licha ya timu yake kucheza mechi mbili za Ligi Kuu Bara na mbili za Ngao ya Jamii, hajashiriki mchezo wowote.

Amekuwa akisumbuliwa na tatizo la goti kwa muda mrefu kitu ambacho baadhi ya mashabiki walianza kuingiwa hofu na utimamu wa mwili wake.

Akizungumzia maandalizi ya mechi hiyo kwa ujumla, Ally amesema kikosi kipo imara na kufanya maandalizi ya nguvu chini ya Kocha, Oliviera Robertinho.

"Msafara wa mashabiki wetu utaanza safari leo saa 12 jion kwenda Ndola, Zambia, na niwaomba mashabiki kuzingatia muda ili tuwahi kufika kwa wakati na kuendelea na maandalizi mengine," amesisitiza Ally.

Simba itatua uwanjani Jumamosi kupimana nguvu na Dynamos katika mchezo utakaosakatwa katika uga wa Levy Mwanawasa mjini Ndola na watarudiana mwishoni mwa mwezi huu jijini Dar es Salaam.