Banyana, Ndoye wa Azam FC kutibiwa Afrika Kusini

KANDANDA Banyana, Ndoye wa Azam FC kutibiwa Afrika Kusini

Na Zahoro Juma • 22:00 - 15.02.2024

Kutokana na hali hiyo nyota hao watakosekana katika mchezo wa kesho dhidi ya Geita Gold

Kiungo mkabaji wa timu ya Azam raia wa Tanzania, Sospter Bajana na mlinzi kati wa timu hiyo, raia wa Senegal, Malickou Ndoye, wanatarajiwa kusafiri kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya kupata matibabu zaidi ya majeraha yanayowasumbua.

Wachezaji hao wawili hawajaonekana uwanjani kwa kipindi kirefu wakiuguza majeraha kitu ambacho kimeulazimu uongozi kuwatafutia matibabu nje ya nchi,

Bajana ambaye ni nahodha msaidizi wa Azam, aliuanza msimu huu kwa kasi lakini alipata majeraha akiwa na timu ya taifa wakati wakijiandaa na michuano ya Afcon ambayo hakufanikiwa kucheza mechi hata moja.

Wachezaji hao wanatarajia kuondoka nchini, Februari 20 kwenda kwenye Mji wa Cape Town ambapo watapatiwa matibabu yao katika Hospitali ya Vicent Pallotti.

"Wachezaji wetu wawili, Bajana na Ndoye wataondoka nchini wiki ijayo kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu zaidi kwa majeraha yanayowasumbua," imesomeka taarifa kutoka katika kurasa rasmi za Klabu ya Azam FC.

Katika hatua nyingine, Klabu ya Azam, kesho itashuka dimbani kuwakaribisha Geita Gold katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaofanyika Azam Complex, Dar es Salaam.

Mchezo huo utakuwa ni wakukamilisha mzunguko wa kwanza kwa kila timu wakati huu ambapo timu nyingine zimeanza kucheza mechi za mzunguko wa pili.

Azam ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi wakiwa na alama 32 huku Geita Gold wakiwa nafasi ya 13 wakiwa na alama 16 baada ya kucheza mechi 14.