Tabora United yaanza kuitafutia 'dawa' Azam FC

Ofisa Habari wa Tabora United, Christina Mwagala

KANDANDA Tabora United yaanza kuitafutia 'dawa' Azam FC

Na Zahoro Juma • 11:44 - 15.02.2024

Timu hiyo ambayo ipo nafasi ya tatu kutoka mkiani ikiwa na alama 16,inajitafuta isishuke daraja

Timu ya Tabora United, imeanza maandalizi kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara ambapo mchezo wao ujao itakuwa dhidi ya Azam FC.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Februali 19 katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mkoani Tabora.

Kikosi hicho cha nyuki wa Tabora, kimeanza mazoezi ikiwa ni mara baada ya kutoka kumaliza mzunguko wa kwanza kwa mchezo dhidi ya Namungo na kutoka sare ya kufungana bao 1-1.

Tabora United chini ya Kocha Mkuu, Goran Copnovic, inaendelea kujifua ili kujiweka vizuri kwenye michezo ya mzunguko huo pamoja na michuano ya Kombe la Azam Sport Federation (ASFC).

“Tumemaliza mzunguko wa kwanza na Namungo na sasa tunajiandaa na mzunguko wa pili ambapo tutakutana na Azam FC Februali 19, na hali ya kikosi iko vizuri hivyo tunazidi kujipanga,” amesema Ofisa Habari wa timu hiyo, Christina Mwagala.

Aidha kwa upande wa afya za wachezaji Mwagala, amesema kuna majeruhi wawili ambao ni Kevin Kingu na Erick Okutu.

Tags: