Tanzania yapanda nafasi mbili viwango FIFA

Wachezaji wa Taifa Stars, Mbwana Samatta (kushoto) na Himid Mao wakati wa michuano ya AFCON

KANDANDA Tanzania yapanda nafasi mbili viwango FIFA

Na Zahoro Juma • 17:33 - 15.02.2024

Hiyo imetokana na ushiriki wao katika michuano ya AFCON 2023 ambapo ilivuna alama 2 katika mechi tatu za hatua ya makundi

Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), limeitaja timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kupanda kwa nafasi mbili katika viwango vya ubora vya Februari, mwaka huu.

Awali Stars ilikuwa ikishikilia nafasi ya 121 duniani lakini kwasasa imesogea hadi nafasi ya 119 huku ikipanda hadi nafasi ya 30 Afrika tofauti na ilivyokuwa mwanzo katika nafasi ya 32.

Stars hivi karibuni imetoka kushiriki michuano ya Afcon iliyofanyika nchini Ivory Coast ambapo waliishia katika hatua ya makundi baada ya kukusanya alama mbili kwenye mechi tatu walizocheza.

Katika michezo yao, Stars walifungwa mabao 3-0 na Morocco kabla ya kulazimisha sare ya 1-1 na Zambia na kisha kutoka suluhu na DR Congo kwenye mchezo wa mwisho.

Mabingwa wa michuano hiyo, timu ya Taifa ya Ivory Coast, wao wamepanda kwa nafasi 10 kidunia ambapo awali walikuwa nafasi ya 49 lakini sasa wamesogea hadi nafasi ya 39.

Hata hivyo kwa Afrika, Ivory Coast wanashika nafasi ya tano nyuma ya Morocco, Senegal, Nigeria na Misri.

Timu ya taifa ya Morocco, licha ya kuishia hatua ya 16 Bora katika michuano ya Afcon lakini imeendelea kuwa kinara katika Bara la Afrika wakifuatiwa na Senegal ambao wapo nafasi ya pili.

Kwa nchi za Afrika Mashariki, Uganda wao wameendelea kushika nafasi ya juu kisoka wakiwa nafasi ya 19 Afrika na nafasi ya 92 duniani wakifatiwa na timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’.

Mabingwa wa Kombe la Dunia, timu ya Taifa ya Argentina, bado ni vinara katika viwango vya ubora duniani wakifuatiwa na Ufaransa na tatu bora ikihitimishwa na Uingereza.

Tags: