Taifa Stars yaanza matizi kambini Misri

KANDANDA Taifa Stars yaanza matizi kambini Misri

Na Zahoro Mlanzi • 19:06 - 03.01.2024

Timu hiyo itakuwa nchini humo kwa siku sita kabla ya kwenda nchini Ivory Coast katika michuano ya AFCON

Kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, kimetua salama nchini Misri na kwenda moja kwa moja kambini na haikuwa na muda wa kupoteza ilianza matizi kuelekea michuano ya Afcon.

Stars iliondoka nchini Tanzania Jumatatu kwa ajili ya kambi ya siku sita nchini Misri kabla ya kuelekea Ivory Coast ambapo michuano ya Afcon itaanza Januari 13.

Wachezaji waliondoka moja kwa moja na timu ikitokea Tanzania walikuwa ni 20 pamoja na benchi la ufundi sambamba na viongozi huku wachezaji wengine tayari wameshaanza kujiunga na timu kambini.

Akizungumza na Pulsesports akiwa nchini Misri, Kocha Msaidizi wa kikosi hicho, Hemed Seleman 'Morocco', amesema walipofika tu timu ilianza mazoezi mara moja kwa ajili ya kuweka miili sawa kabla hawajaanza mazoezi ya kimbinu.

Ameongeza kwa kusema kikosi kinazidi kupokea nyota kutoka sehemu mbalimbali ambao walikuwa bado hawajaungana na timu wakati ipo Tanzania.

"Hadi sasa timu inazidi kusheheni wachezaji wetu ambao walikuwa bado hawajaungana na sisi, tumempokea Himid Mao, Charles M'mombwa na Khelfin Salum 'Fini'," amesema.

Wakiwa nchini Misri, timu hiyo inatarajia kucheza mechi moja ya kirafiki kabla ya Januari 8 kuondoka kwenda Ivory Coast.

Stars itatupa karata yao ya kwanza katika michuano hiyo wakiwa Kundi F, Januari 17 kwa kucheza na Morocco. Baada ya mchezo huo itashuka tena dimbani Januari 21 kucheza na Zambia kisha itamaliza ratiba ya makundi Januari 24 kwa kucheza na DRC.

Tags: