Simba Queens yaichapa Yanga Princess 3-1

KANDANDA Simba Queens yaichapa Yanga Princess 3-1

Na Zahoro Mlanzi • 19:32 - 03.01.2024

Mchezo huo ni wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara ukiwa ndio mzunguko wa tatu tangu kuanza kwa msimu wa 2023/24

Kikosi cha timu ya Simba Queens, kimeibuka na ushindi wa mabao 3-1 mbele ya mahasimu zao Yanga Princess katika mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Mabao ya Simba Queens katika mchezo huo, yamefungwa na Aisha Mnuka aliyefunga mawili kabla ya mapumziko huku bao pekee la Yanga lilifungwa kupitia kwa Neema Paul na kufanya timu hizo kwenda kupumzika matokeo yakiwa 2-1.

Kipindi cha pili, Simba Queens walianza kwa kasi kama ilivyokuwa kipindi cha kwanza na kasi yao iliwalipa kwa kuongeza bao la tatu kupitia kwa kiungo wao, Vivian Corazone.

Kwa matokeo hayo, Simba Queens imefikisha alama 9 na kubakia nafasi ya pili kwenye msimamo nyuma ya vinara JKT Queens kwa tofauti ya mabao.

Yanga Princess wao wamesalia na nafasi ya tatu na alama zao 6 baada ya mechi tatu.

Ushindi huo ni mwendelezo kwa Simba Queens kuwatambia Yanga Princess kwani walianza katika michuano ya Ngao ya Jamii iliyofanyika mwezi uliopita.

Katika mchezo huo, Simba Queens ilishinda Kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya dakika 90 kutoka suluhu.

Tags: