Kocha Benchikha afanya kikao na wachezaji Simba SC

LIGI KUU Kocha Benchikha afanya kikao na wachezaji Simba SC

Zahoro Mlanzi • 09:36 - 30.11.2023

Amekutana na wachezaji wake kwa mara ya kwanza tangu apewe majukumu ya kuinoa timu hiyo kwa mkataba wa miaka 2

Kocha mpya wa timu ya Simba SC, Abdelhak Benchikha raia wa Algeria, amekutana kwa mara ya kwanza na wachezaji wake na kufanya nao kikao maalum.

Kocha huyo jana alitambulishwa rasmi kwa mashabiki na wanachama wa timu hiyo na kuahidi kuanza na mambo matatu ili kurudisha makali ya timu hiyo.

Benchikha ambaye amepewa kandarasi ya miaka miwili, amerithi mikoba iliyoachwa na Mbrazil Roberto Oliviera 'Robertinho' aliyetimuliwa hivi karibuni ndani ya timu hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtandao wa kijamii wa X wa klabu hiyo, imewaonesha benchi lote jipya la ufundi likiongozwa na Benchikha wakiwa katika kikao maalum.

Taarifa hiyo imeonesha wachezaji hao kila mmoja alipata fursa ya kujitambulisha kwa kusimama na kutoa maelezo binafsi na baada ya hapo waliendelea na programu zingine.

Makocha wengine waliokuwepo katika kikao hicho ni Farid Zemiti ambaye ni Kocha Msaidizi pamoja na Kamal Boujdjenane ambaye ni Kocha wa Viungo.

Kocha huyo kibarua chake cha kwanza kitakuwa ugenini dhidi ya Janweng Galaxy ya Botswana katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi utakaopigwa Desemba 2 nchini humo.

Anajiunga na Simba akiwa anatokea Klabu ya USM Alger ambayo msimu uliopita aliwasaidia kushinda taji la Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuwafunga Yanga katika mchezo wa fainali.

Pia Benchikha ameisaidia USM Alger kushinda ubingwa wa Super Cup ambapo aliwafunga Al Ahly katika mchezo uliofanyika Saudi Arabia

Tags: