Kocha Al Ahly amtupia lawama mwamuzi sare 2-2 na Simba

© Kwa Hisani

KANDANDA Kocha Al Ahly amtupia lawama mwamuzi sare 2-2 na Simba

Zahoro Mlanzi • 15:00 - 21.10.2023

Katika mchezo huo, Al Ahly ndio walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Reda Slim aliyefunga dakika za majeruhi kabla ya mapumziko.

Kocha wa Klabu ya Al Ahly, Marcel Koller, amemtupia lawama mwamuzi Beida Dahane kwa madai ya kushindwa kuwapa mkwaju wa penalti kwenye mechi ya ufunguzi ya michuano ya AFL dhidi ya Simba ambapo mchezo huo ulipigwa Uwanja Mkapa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya 2-2.

Akizungumza na vyombo vya habari, Koller ambaye timu yake ilipata sare hiyo baada ya kusawazisha kipindi cha pili kupitia kwa Mahmoud Kahraba, amesema katika kipindi cha kwanza licha ya kuwa walicheza vizuri na kupoteza nafasi za kufunga lakini walistahili penalti ambayo mwamuzi wa kati raia wa Mauritania alikataa.

"Timu yangu ilikuwa bora kwenye kipindi cha kwanza, tulitengeneza nafasi za kufunga hatukuzitumia na baadaye tukanyimwa penalti ambayo kwa upande wangu naona ilistahili tuipate, sijui kwanini mwamuzi ameikataa licha ya kuangalia kwenye VAR," amesema.

Katika mchezo huo, Al Ahly ndio walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Reda Slim aliyefunga dakika za majeruhi kabla ya mapumziko.

Hata hivyo mara baada ya kuanza kipindi cha pili Simba walisawazisha kupitia kwa Kibu Denis na kisha Sadio Kanoute kuongeza la pili kwenye dakika ya 57.

Matokeo ya sare ya 2-2 yanaiweka katika mazingira mazuri Al Ahly ambayo Jumanne watakuwa nyumbani kuwakaribisha Simba kwenye mechi ya marudiano na mshindi wa jumla atavuka kwenda hatua ya nusu fainali.

Wakati huohuo, kikosi cha Al Ahly, kimeondoka nchini Tanzania na kurudi kwao Misri kwa ajili ya kwenda kujiandaa na mchezo wa marudiano dhidi ya Simba mechi ambayo itachezwa Oktoba 24 kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo.