Waogeleaji wanne kuiwakilisha Tanzania mashindano ya Dunia Qatar

KUOGELEA Waogeleaji wanne kuiwakilisha Tanzania mashindano ya Dunia Qatar

Zahoro Juma • 15:33 - 23.01.2024

Nyota hao wataondoka nchini Februari 8 tayari kwa ajili ya mashindano hayo yatakayoshirikisha mataifa mbalimbali

Wachezaji wanne, wanatarajia kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Dunia ya kuogelea ambayo yataanza Februari 11 hadi 18 mwaka huu mjini Doha, Qatar.

Wachezaji hao wanatarajia kuondoka nchini Februari 8, mwaka huu na kurejea nchini Februari 19.

Akizungumza wakati wa kuwataja waogeleaji hao jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Inviolata Itatiro amesema kati ya hao wawili ni wasichana na wengine wakiume.

Amewataja waogeleaji hao wakike ni Natalia Ladha, Amylia Chali na kwa wakiume ni

Michael Joseph na Prince Alimanya ambapo watakuwa chini ya Kocha wa timu ya Taifa, Michael Mwakipesile.

Ameongeza malengo ya kushiriki mashindano hayo ni pamoja na kuongeza uzoefu, uwezo katika anga ya kimataifa, fahari ya utaifa ambao utawaongezea ari na motisha kwa vijana wengi zaidi kushiriki katika mchezo huo na kuongeza ushindani.

Amebainisha malengo mengine ni maendeleo ya vipaji ambayo yatasaidia kipima viwango vya waogeleaji katika anga ya kimataifa na kutengeneza utamaduni wa mafunzo endelevu.

Katika msafara huo, kutakuwa na viongozi watatu ambao ni Mwenyekiti, David Akim na Katibu Mkuu, Inviolata pamoja na Mjumbe wa Shirikisho la Afrika Tanzania, Thauriya Diris ambapo wanatarajia kushiriki Mkutano Mkuu wa Dunia ambao inaweza kuleta chachu katika mchezo wa kuogelea.

Tags: