Tanzania, Uganda na Kenya kuaandaa AFCON 2027

©Hisani

KANDANDA Tanzania, Uganda na Kenya kuaandaa AFCON 2027

Zahoro Mlanzi • 16:12 - 27.09.2023

Tanzania, Kenya, na Uganda zimechaguliwa na CAF kuandaa AFCON 2027, kupitia ombi lao la Pamoja BID, kwa mara ya kwanza.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limepitisha mataifa ya Tanzania, Kenya na Uganda kuandaa michuano ya AFCON 2027.

Nchi hizo ziliwasilisha ombi walilolipa jina la Pamoja BID na itakuwa ni mara ya kwanza Ukanda wa Afrika Mashariki kuandaa michuano hiyo mikubwa ya soka Afrika.

Pamoja Bid imeshinda mbele ya Algeria, Botswana na Misri ambazo zilionesha nia ya kuandaa michuano hiyo kwa mwaka huo.

Kamati ya Utendaji CAF, imetangaza uamuzi huo jijini hapa, pia Morocco imechaguliwa kuandaa AFCON 2025 kutokana na Guinea kupoteza sifa kwa kuwa nyuma katika maandalizi.

Morocco imeyashinda mataifa kama Algeria, Zambia na muunganiko wa Benin na Nigeria.

Kwa Kenya itakuwa ni mara ya pili kujaribu kuomba kuwa mwenyeji baada ya ombi la kwanza mwaka 1996 kukubaliwa, lakini baadaye wakapokonywa na kuhamishiwa Afrika Kusini.

Mwaka 2017, Kenya iliomba tena uenyeji lakini ni kwa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) ombi ambalo lilikubaliwa ila kwa mara ya nyingine tena wakapokonywa na michuano hiyo kuhamishiwa Rwanda.

Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo wa Tanzania, Dkt. Damas Ndumbaro, aliondoka nchini kwenda Misri kwa ajili ya kupiga chapuo jambo hilo ambalo linaungwa mkono kwa karibu na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na marais Yoweri Museveni wa Uganda na Dkt. William Ruto wa Kenya.

Tags: