Lomalisa aanza matizi Yanga

KANDANDA Lomalisa aanza matizi Yanga

Na Zahoro Mlanzi • 16:24 - 18.12.2023

Yanga imepata nafuu baada ya beki wa kutegemewa Joyce Lomalisa kurudi mazoezini

Kikosi cha timu ya Yanga SC, kimerejea tena mazoezini huku taarifa njema kwa Kocha, Miguel Gamondi ni kurudi uwanjani kwa mlinzi wake wa kushoto raia wa DRC, Joyce Lomalisa.

Lomalisa ameumia Desemba 2 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam wakati timu yake ikikabiliana na Al Ahly wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika na baada ya hapo akakosekana katika mechi mbili zilizofuata ambazo ni dhidi ya Medeama na Mtibwa Sugar iliyofanyika Jumamosi.

Yanga wanajiandaa na mchezo wa mzunguko wa nne wa hatua ya makundi ya Afrika ambapo kesho inatarajia kuikaribisha Medeama SC kutoka Ghana Uwanja wa Mkapa kuanzia saa 10 jioni.

Akizungumza na Pulse Sports, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, amesema baada ya kuifunga Mtibwa Sugar 4-1, mwishoni mwa wiki wachezaji hawakupewa muda wa mapumziko badala yake waliendelea kukaa kambini kwa ajili ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Medeama.

Kamwe amesema Lomalisa alikuwa ni miongoni mwa wachezaji ambao wanafanya mazoezi na timu na kama kocha ataridhika naye basi atapewa nafasi ya kucheza Jumatano.

"Wachezaji wote wapo kambini wakiendelea na maandalizi akiwemo Lomalisa ambaye alikuwa majeruhi, kwasasa anaendelea vizuri na kama itampendeza kocha basi atatumika," amesema Kamwe.

Tangu kuumia kwa Lomalisa nafasi yake imekuwa ikichezwa na mlinzi mzawa, Nickson Kibabage ambaye alionekana kumudu vyema eneo hilo.