Yanga SC yaipiga Medeama 3-0 michuano ya Afrika

KANDANDA Yanga SC yaipiga Medeama 3-0 michuano ya Afrika

Na Zahoro Mlanzi • 19:45 - 20.12.2023

Ushindi huo umefufua matumaini ya timu hiyo kufuzu robo fainali ambapo sasa imefikisha alama 5 sawa na Al Ahly ya Misri

Timu ya Yanga SC, imefufua matumaini ya kucheza hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuichapa Medema SC kwa mabao 3-0.

Mchezo huo ambao ulipigwa Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam, umeifanya Yanga kupanda hadi nafasi ya pili ikiwa na alama 5 sawa na Al Ahly ya Misri ila zinatofautiana kwa mabao huku Medeama akibaki na alama zao 4.

Hata hivyo, Al Ahly itakuwa na kibarua kigumu uwanjani kwa kuumana na CR Belouzdad yenye alama 4 katika mchezo mwingine wa Kundi D ambao utapangiwa siku kutokana na miamba huyo ya Misri kuwa katika majukumu mengine.

Mabao ya Yanga katika mchezo huo, yamefungwa na Pacome Zouzoua, Bakari Mwamnyeto na Mudathir Yahya.

Katika mchezo huo ambao ulihudhuriwa na maelfu ya mashabiki, Yanga ingeweza kumaliza mchezo tangu dakika 45 za kwanza kutokana na nafasi zilizotengenezwa ila walishindwa kuzitumia.

Kiungo Max Nzengeli, straika Kennedy Musonda na Mudathir kama wangekuwa makini zaidi basi wangeenda mapumziko kwa kuiwezesha timu yao ya Yanga kuwa mbele kwa mabao 3-0.

Medeama itajutia zaidi nafasi iliyopata mwanzoni mwa kipindi cha pili ya mkwaju ya penalti lakini straika wao, Jonathan Sowah alimlenga kipa, Djigui Diarra aliyepangua na mpira kutoka pembeni ya goli.

Hata hivyo Sowah hakumaliza mchezo huo baada ya kuoneshwa kadi ya pili ya njano dakika ya 89 na Mwamuzi, Redouane Jiyed kutokana na mchezo usio wa kiungwana aliofanya dhidi ya Mahlatse Makudubela 'Skudu' na kutolewa nje kwa kadi nyekundu.

Pacome amefungua kalamu hiyo ya mabao dakika ya 32 kwa kuwakimbiza wachezaji wa Medeama karibu ya katikati ya uwanja hadi kwenda kufunga bao hilo liliwapa nguvu wachezaji wa wenzake.

Nahodha Mwamnyeto amefunga bao la pili dakika ya 60 kwa kichwa akiunganisha mpira wa kichwa uliopigwa na Musonda aliyeitendea haki krosi ya Kouassi Yao.

Bao la ushindi la Yanga, limefungwa baada ya wachezaji wa timu hiyo kupiga pasi nyingi na kuwazubaisha Medeama ambapo walifanya shambulizi la kushtukiza ambapo Stephane Aziz KI alipiga pasi nzuri iliyotua miguu mwa Mudathiri aliyekwamisha mpira wavuni.

Baada ya mchezo huo, Yanga sasa itasafiri kwenda mkoani Tabora kuumana na Tabora United katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Ijumaa.

Tags: